Moja ya shida ambayo watu ambao hawajafanya maamuzi ya mafanikio wanaipata, ni kuibuka kwa njia za mkato kila siku.
Wote tunajua kabisa kwamba hakuna mafanikio yanayopatikana kwa njia ya mkato. Wote tunajua kazi na muda vinahitajika ili mtu aweze kufanikiwa. Wote tunajua safari ya mafanikio inahusisha kushindwa mara nyingi.
Lakini watu wanakuja na njia mpya, wanakuambia hii ni tofauti, siyo sawa na zile ulizosikia siku za nyuma. Hii ni ya uhakika, ni ya mkato na huhitaji kuweka kazi. Mafanikio ni nje nje.
Halafu mtu unafikiria, labda inaweza kuwa kweli, kwa nini nisijaribu tu, kama ni kweli halafu sikujaribu si nitakuwa nimekosa fursa nzuri. Unajiambia tena, hata hivyo kufanikiwa lazima uwe ‘risk taker’. Unaingia kichwa kichwa, unapogwa na wajanja wananufaika kupitia wewe.
Swali unaloweza kujiuliza, kama njia hizi za mkato hazifanyi kazi, kwa nini kila siku zinakuja njia mpya?
Kabla sijakujibu, kila siku wapo watu wanaojiuza, wanauza miili yao ya ngono, je unafikiri kwa nini watu wanajiuza? Jibu, ni kwa sababu wapo wanaonunua. Kama pasingekuwa na wanunuzi, biashara ya watu kujiuza ingeisha mara moja.
Na hilo ndiyo jibu la kwa nini njia mpya za mkato zinaibuka kila siku. Ni kwa sababu wapo watu wanaozitafuta, sasa wajanja wakijua watu wanataka mkato, wanawatengenezea mkato ambao wao wenyewe wanajua haufanyi kazi, lakini utawanasa wenye tamaa ya njia za mkato.
Hivyo njia pekee ya wewe kuepuka mitego hii, ni kufanya maamuzi na maisha yako, kwamba kamwe hutakuja kujaribu njia yoyote ya mkato. Fanya maamuzi unataka nini na maisha yako na utafanya nini kupata unachotaka na fanya hivyo, usiangalie kabisa wengine wanasema au kufanya nini.
Na mtu anapokuja kwako na njia ya mkato, wala hata usimsikilize, achana naye na kazana kufanya kazi zako. Na nakuhakikishia, ukiwa ‘bize’ na kufanya kazi yako, wala hakuna atakayekusogelea na ujinga huo wa njia za mkato.
Ukiona unaanza kufikiria labda njia fulani ya mkato inaweza kuwa sahihi, jua hufanyi kazi, na hivyo umeanza kuyumba kutoka kwenye lengo lako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,