Upo usemi maarufu kuhusu biashara kwamba biashara ni ushindani. Sasa kama utaubeba usemi huo na kuingia kwenye biashara kwa kuamini kwamba unaweza kushindana, unaweza ukashinda, lakini utabaki na ushindi usio na maana.
Ushindi pekee unaohitaji kwenye biashara ni faida. Na faida ni pale gharama zako zote mpaka mteja anapata anachotaka, zinakuwa ndogo kuliko mapato unayoingiza.
Chochote nje ya hapo ni usumbufu kwako na biashara yako. Kushindana na wengine ili tu biashara yako ionekane ipo juu ni kupoteza muda wako na nguvu zako.
Ushindi pekee na wenye maana ni faida, kama hupati faida, hata kama unauza kuliko wengine, unajulikana kuliko wengine, huna maana. Si muda mrefu utapotea kabisa kwenye biashara hiyo.
Lakini pia huwezi kuwazuia watu wasifanye biashara ambayo unafanya, na chochote unachofanya kwenye biashara yako, wengine wanaona na watafanya kwenye biashara zao.
Na hapa ndipo unapohitaji kutengeneza uhodhi wako binafsi. Wazungu wanaita MONOPOLY OF YOU. Yaani unahitaji kuwa kwenye biashara yako, kwa namna ambayo hakuna mwingine anaweza kuwa. Unahakikisha kuna aina ya huduma ambayo mteja anapata kwako tu, na hata aende pengine wapi, hawezi kuipata kamwe.
Hichi ndiyo unahitaji kwenye biashara yako ili uache kushindana na uanze kushinda kwa kutengeneza faida. Kama biashara yako haina kitu cha aina hiyo, hujaanza biashara bado. Rudi mezani na nenda katengeneze uhodhi wako binafsi, ni kitu gani hasa utahodhi kwa wateja wako kiasi kwamba hawataweza kwenda pengine?
Kila mtu na kila biashara ina kitu cha aina hii. Jua kwenye biashara yako na anza kufanyia kazi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,