Rafiki yangu mpendwa,

Katika ugunduzi bora kabisa wa binadamu kwenye muda, ukiondoa saa basi ni kupanga muda kwenye juma lenye siku saba.

Mpango wa asili wa muda ni usiku na mchana, mipango mingine yote imetengenezwa na wanadamu. Kwamba kuna wiki, mwezi, mwaka, muongo, karne na hata milenia, yote hiyo ni mipango yetu wanadamu.

Wiki ndiyo mpango bora sana wa muda kwa sababu unaweza kuzipangilia na kuzisimamia vizuri siku saba. Unaweza kuchukua hatua ya kubadili kile ambacho hakiendi vizuri. Japo unahitaji kuwa na mipango ya muda mrefu, ya miaka mingi, unahitaji kuchukua hatua kwa juma.

Ndiyo maana kila mwisho wa juma nimekuwa nakukumbusha kufanya vitu viwili muhimu. Cha kwanza ni kupitia juma unalomaliza, kuangalia yale uliyofanya na yale uliyoshindwa. Cha pili ni kupangilia juma unalokwenda kuanza, yapi utafanya, huku ukizingatia uliyojifunza kwenye juma lililopita.

Ukiweza kusimamia vizuri kila juma lako, utaweza kuyasimamia vizuri sana maisha yako.

Karibu tena rafiki yangu kwenye tano za juma, ambapo nakushirikisha mambo matano muhimu ya kujifunza na kufanyia kazi kwenye maisha yako. Mkusanyiko huu wa mambo matano siyo tu wa kujifurahisha kujua, bali kutafakari kwa kina na kwenda kuanza juma jipya ukiwa na hatua bora zaidi za kuchukua.

Yafuatayo ni mambo matano muhimu sana niliyokuandalia kwa juma hili la 32 ili unapokwenda kuanza juma la 33 la mwaka huu 2018, liwe juma bora sana kwako.

#1 KITABU NILICHOSOMA; TAHAJUDI KWA LUGHA RAHISI KUELEWA.

Lugha inahusika sana kwa namna ambavyo watu wanaelewa na kuchukua hatua kwenye kitu. Na falsafa yangu kwenye uandishi na ufundishaji imekuwa ni kueleza kitu kwa lugha rahisi kiasi kwamba mwanafunzi wa darasa la tano anaweza kuelewa vizuri na akachukua hatua.

Tahajudi au kama wengine wanavyoita taamuli na kwa kiingereza MEDITATION ni kitu ambacho kila mtu amekuwa na lake la kusema. Kuanzia kwamba ni nini, faida zake na hasara zake, ufanyaji wake na hata jinsi ya kukua zaidi kupitia tahajudi, wengi wamekuwa wanajiona kama wapo kwenye giza.

Na kama ilivyo kwetu binadamu, tusipoelewa kitu tunakipuuza na kuachana nacho hata kama kina manufaa makubwa kwetu.

Mwandishi na mwalimu wa kiroho Bhante Gunaratana alichukua muda wa kuandika mwongozo wa tahajudi kwa lugha rahisi sana kueleweka na yeyote yule. Mwongozo huu ni kitabu alichokiita MINDFULNESS IN PLAIN ENGLISH.

mindfulness in plain english

Kwenye kitabu hichi, mwandishi anatuambia tahajudi ni nini na pia siyo nini, kwa sababu yapo mengi sana yanasemwa kuhusu tahajudi ambayo siyo sahihi. Anatushirikisha jinsi ya kupanga kufanya tahajudi, kuanzia nguo za kuvaa, mkao mzuri na hata muda gani wa kutahajudi na utahajudi kwa muda gani. Pia mwandishi ametushirikisha jinsi ya kutatua changamoto tunazokutana nazo wakati wa kutahajudi na hata jinsi ya kuepuka kelele zisituzuie kutahajudi. Mwisho kabisa mwandishi ametueleza aina mbalimbali za tahajudi kama tahajudi ya kutembea.

Naweza kusema, kwa yule asiyejua kwa nini anapaswa kufanya tahajudi, maana hichi ni kitu kila mtu anapaswa kufanya, basi kitabu hichi ni mwongozo mzuri sana kwake.

Hapa nitakushirikisha maeneo matatu muhimu ambayo kila mtu anapaswa kuyajua kuhusu tahajudi.

ENEO LA KWANZA; TAHAJUDI NI NINI?

Tahajudi ni njia ya kuituliza akili kwa kudhibiti mawazo ambayo mtu anayo na kuweza kuwa na utambuzi sahihi juu yake na mazingira ambayo yanamzunguka. Watu wengi tunafanya vitu, lakini hatuvifanyi kwa uelewa. Kwa mfano mtu anaweza kuwa anakula huku anafikiria kazi, anafanya kazi huku anafikiria kupumzika na kadhalika.

Mawazo yetu yamekuwa yanachukuliwa kama nyani, ambaye anaruka ruka kutoka tawi moja la mti kwenda tawi jingine. Ndani ya muda mfupi unaweza kuwa na mawazo mengi sana, kiasi cha akili yako kuchoka na usiweze kufanya chochote unachofanya kwa umakini.

Na kwa dunia ya sasa, dunia yenye kelele za kila aina, na kelele tunatembea nazo popote tulipo, watu wamevurugwa kuliko wakati wowote ule. Maana mtu anaweza kufanya kitu kidogo, akikutana na ugumu anakimbilia kuangalia simu yake, anaingia mtandaoni, anawasiliana na watu na kadhalika.

Tahajudi inatusaidia kuweza kudhibiti akili na mawazo yetu, kuweza kuweka umakini kwenye chochote tunachofanya na kuacha kuendeshwa kwa hisia na matukio na badala yake kuwa na utulivu kwenye chochote ambacho mtu umechagua kufanya.

Budha, ambaye ndiye muasisi wa falsafa na dini ya ubudha, ambayo ndiyo inahusishwa zaidi na tahajudi, alikuwa akirudia sana kauli hii; KIINI CHA MAISHA NI MATESO. Kauli hii japo wengi hawapendi kuikubali, ni sahihi kwa kila aina ya maisha. Haijalishi mtu ana nini kwenye maisha yake, kwa namna moja au nyingine kuna maumivu na mateso ambayo anakutana nayo. Hata kama mtu kwa nje anaonekana ana raha kiasi gani, ndani yake kuna maumivu fulani.

Sasa kosa ambalo wengi wamekuwa wanafanya, ni kujaribu kuficha maumivu na mateso yao. Wanafanya hivyo kwa kukazana kununua vitu vizuri zaidi vinavyoonekana kwa nje na kuwapa hadhi fulani kwenye jamii, kama nguo, magari na mali mbalimbali. Wengine wamekuwa wanaficha maumivu na mateso yao kwa kutumia vilevi kama pombe na madawa ya kulevya.

Lakini kama wote tunavyojua, licha ya kufanya vyote hivyo, bado maumivu na mateso hayaondoki, badala yake yanazidi kuwa makubwa zaidi. Ndiyo maana utakuta mtu anazidi kununua vitu zaidi na kusema utajiri hauleti furaha. Au mtu anazidi kuwa mlevi zaidi akifikiri ndiyo njia ya kuondokana na maumivu hayo.

Kupitia tahajudi, unayafunua kila maumivu na mateso yaliyopo ndani yao, kwa kuanza kujitenga nayo na kuyaangalia kisha kupata suluhisho sahihi la mateso na maumivu hayo.

Kauli nyingine ambayo Buddha anatuambia ni maumivu ni lazima, lakini mateso ni kuchagua. Pale unapokuwa na uelewa wa maumivu yako, unachagua kutokuteseka na kuchukua hatua sahihi kupata ufumbuzi. Lakini kama hutayajua maumivu, utaendelea kuwa na maisha ya mateso muda wote.

ENEO LA PILI; IMANI POTOFU KUHUSU TAHAJUDI.

Kumekuwa na imani nyingi potofu kuhusiana na tahajudi, kila mtu akisema lake, hasa wale wasiokuwa na uelewa sahihi.

Mwandishi amechukua muda kutueleza imani potofu 11 kuhusiana na tahajudi. Hapa nitakutajia imani hizo potofu ili kama ulishasikia au kufikiri hivyo uache mara moja.

 1. Tahajudi siyo zoezi la kuondokana na uchovu. Japo moja ya faida utakazopata kwa kufanya tahajudi ni kuondokana na uchovu, lakini hilo siyo kusudi la tahajudi. Kusudi kuu ni kupata utambuzi kamili wa maisha yako.
 2. Tahajudi siyo zoezi la kukuwezesha kusafiri kiroho. Japo wapo watu wanaoweza kutumia tahajudi kusafiri kiroho, hilo siyo lengo kuu kwako kufanya tahajudi.
 3. Tahajudi siyo kitu kigumu na kisichoeleweka kama wengi wanavyoamini. Ni zoezi rahisi ambalo kila mtu anaweza kufanya na akapata manufaa yake.
 4. Tahajudi siyo njia ya mtu kupata uwezo mkubwa wa kiroho wa kutabiri na hata kuona maisha ya wengine kama wapiga ramli. Wapo wanaoweza kufikia ngazi hiyo kupitia tahajudi, lakini siyo lengo kuu la tahajudi.
 5. Tahajudi siyo zoezi hatari ambalo mtu asiye na imani dhabiti anapaswa kuliepuka. Kuna ngazi za tahajudi na yeyote anaweza kuanzia ngazi ya chini.
 6. Tahajudi siyo kwa ajili ya watu wa dini na watakatifu pekee. Ni zoezi ambalo kila mtu anaweza kufanya.
 7. Tahajudi siyo kukimbia uhalisia, badala yake ni kuukabili uhalisia kwa undani zaidi.
 8. Tahajudi siyo njia rahisi ya kupata raha kwenye maisha. Japo kupitia tahajudi unaweza kupata raha fulani, lakini siyo kwa urahisi kama wengi wanavyofikiri.
 9. Tahajudi siyo ubinafsi, kwa sababu unatenga muda wa kukaa mwenyewe na kutafakari haimaanishi ni mbinafsi, badala yake kwa kuwa bora wewe, unawasaidia wengine nao kuwa bora pia.
 10. Unapotahajudi hukai tu chini na kutengeneza fikra usizokuwa nazo, badala yake unazichunguza fikra ambazo tayari unazo na kuweza kuzituliza zisichoshe akili yako.
 11. Kufanya tahajudi kwa muda mfupi hakutaondoa matatizo yako yote ya maisha. Tahajudi siyo tiba ya haraka ya matatizo ya maisha yako. Umekuwa na miaka mingi ya kutengeneza matatizo yako, hivyo tahajudi itakuchukua muda pia.

Imani hizi potofu kuhusu tahajudi zimekuwa zinawatisha wengi na hata kuwakatisha tamaa wengine na kuona hicho siyo kitu kinachowafaa. Ondokana na imani hizo na anza zoezi la tahajudi kila siku kama ninavyokushirikisha hapo chini.

ENEO LA TATU; JINSI YA KUFANYA TAHAJUDI.

Kwanza kabisa unahitaji eneo la kuelekeza mawazo yako. wapo wanaochagua maneno ya kusema, wapo wanaochagua picha ya kuangalia. Lakini njia rahisia ambayo kila mtu anaweza kutumia ni kuelekeza mawazo yake kwenye pumzi zake. Peleka mawazo yako yote kwenye pumzi zako, unaweza kufanya hivyo kwa kuhesabu moja unapovuta pumzi, kisha mbili unapotoa pumzi. Kwa kufanya hivi kuna wakati mawazo yako yatakuponyoka na ukaanza kufikiria vitu vingine. Unachohitaji ni kuyarudisha kwenye pumzi zako.

Pili chagua muda ambao utakuwa unafanya tahajudi. Asubuhi na mapema, ni muda mzuri kwa sababu kunakuwa na utulivu. Pia usiku kabla ya kulala ni muda mzuri wa kupumzisha akili yako baada ya mikiki ya siku nzima.

Tatu chagua eneo utakalokuwa unafanyia tahajudi. Chagua eneo tulivu ambapo hutakuwa na usumbufu wa aina yoyote, pia hakutakuwa na watu wanaokusumbua kiasi cha wewe kushindwa kutuliza mawazo yako. Hapa kwenye eneo, weka mazingira mazuri kwako kuweza kukaa bila ya kuumia. Kama unakaa chini basi kuwe na kitu unatandika ili unapokaa kwa muda mrefu usiumie.

Nne panga urefu wa muda utakaofanya tahajudi. Kwa kuanza tenga dakika 20 mpaka 30 za kukaa na kutahajudi. Kama unashindwa chagua dakika 5 mpaka 10 za kufanya tahajudi kisha endelea kuongeza muda kadiri unavyokwenda. Lengo ni uweze kukaa kwa angalau saa moja kila unapofanya tahajudi. Kitu ambacho kitakusaidia sana.

Tano fanya tahajudi, utajifunza tahajudi kwa kufanya, siyo kwa kusoma. Fuata yale uliyopanga, kwa muda uliotenga na eneo ulilopanga kufanyia tahajudi. Kaa chini na elekeza mawazo yako kwenye pumzi zako. Mwanzoni zoezi litakuwa gumu, lakini usikate tamaa, endelea kurudisha mawazo yako kwenye pumzi zako na usikubali usumbufu wowote ukutoe hapo. Kwa kuanzia unaweza kuweka alamu itakayokupa ishara dakika ulizotenga zimeisha. Na usiache mpaka pale alamu itakapokuambia muda umeisha.

Anza kufanya tahajudi sasa, na kama unahitaji kujifunza zaidi soma kitabu hichi na vingine vinavyoelezea tahajudi. Pia kama upo kwenye KISIMA CHA MAARIFA, unaweza kuuliza swali lolote kuhusu tahajudi na nikakujibu ili uweze kufanya kwa ubora zaidi.

#2 MAKALA YA WIKI; KITU KIMOJA MUHIMU SANA KWAKO KUNUNUA.

Kuna kitu muhimu sana kwenye maisha ya yeyote anayetaka kufanikiwa. Lakini nimekuwa naona baadhi ya watu wanakosa kipaumbele kwenye kununua kitu hicho. Kwenye makala ya wiki hii nilikushirikisha mfano wa rafiki yangu mmoja aliyeshindwa kununua kitu hicho muhimu na jinsi inamgharimu. Unaweza kusoma makala hiyo hapa; Kama Huwezi Kutoa Fedha Yako Na Kununua Kitu Hichi Kimoja, Unajizuia Wewe Mwenyewe Kufanikiwa.

Pia niliandika makala ya vitu vitatu usivyojua kuhusu fedha ambavyo vinakufanya ushindwe kufika kwenye utajiri. kama hukusoma makala hiyo, isome hapa pia; Vitu Hivi Vitatu Usivyovijua Kuhusu Fedha Ndiyo Vinakuzuia Wewe Kufika Kwenye Utajiri Na Uhuru Wa Kifedha.

#3 TUONGEE PESA; UBAYA WA FEDHA NI USIPOKUWA NAZO.

Hivi umewahi kugundua kwamba watu wasiokuwa na fedha ndiyo wanaoongoza kwa kusema vibaya kuhusu fedha? Na hapo unapata jawabu kwa nini hawana fedha. Kwa sababu chochote unachokisema vibaya, kinakukimbia.

Rafiki yangu, ubaya wa fedha ni pale usipokuwa nazo. Kwa sababu utakuwa unahitaji sana kufanya baadhi ya vitu, lakini fedha huna. Hapo utapata hasira, utaona labda wewe hupati fedha kwa sababu wenye nazo wanakuzuia wewe usipate.

Ukweli kwenye fedha unabaki kwamba hakuna anayekuzuia kuzipata, ni mawazo yako mwenyewe na chuki zako kwa wenye nazo.

Anza kuwapenda wenye fedha, anza kutoa thamani kubwa kwa wengine na usijisikie vibaya kuwaambia wengine wakulipe zaidi kwa thamani unayotoa.

Hakuna ubaya wowote kwenye fedha, mpaka pale unapokuwa huna fedha na maisha yanakuwa magumu kwako. Usiwe na hasira na yeyote, bali chukua hatua kuhakikisha unatengeneza kipato cha kukuwezesha kuendesha maisha yako kwa namna unavyotaka yaende.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; ZIMEBAKI SIKU 80 TU, CHUKUA HATUA SASA.

Rafiki, nakukumbusha zimebaki siku 80, miezi kama mitatu na majuma 11 mpaka kufikia tarehe ya mwisho ya kulipia ili kuweza kushiriki tukio kubwa kabisa la mwaka huu 2018 ambalo ni SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018.

Semina itafanyika Dar es salaam na ada ya kushiriki semina hii, ambayo itahusisha huduma zote za siku ya semina ni shilingi 100,000/=. Semina itafanyika jumamosi ya tarehe 03/11/2018. Mwisho wa kulipa ada hii ya kushiriki ni tarehe 31/10/2018. Na pia unaweza kulipa kidogo kidogo kadiri unavyoweza wewe. Kuanzia elfu moja kwa siku, elfu 10 kwa wiki au elfu 30 kwa mwezi. Nitapokea na kuweka kumbukumbu zako ili usikose semina hii muhimu sana kwako.

Ili kuhakikisha unaendelea kupata taarifa za semina hii, nimeandaa kundi maalumu la wasap kuhusu semina. Naomba kama tu utashiriki semina hii basi ujiunge. Kama unajua hutashiriki usijiunge, ili wale wanaoshiriki wapate nafasi. Kujiunga na kundi hili, bonyeza kiungo hichi hapa; https://chat.whatsapp.com/L3F4jaeYcZO4drSCxWYrPr

Karibu sana kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, tushirikishane yale muhimu sana kwenye safari yetu ya mafanikio.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KINACHOWAFANYA BAADHI WAWEZE KUFANYA MAKUBWA.

“They can because they think they can.” – Virgil

Kuna watu ambao wanaonekana wanaweza kufanya makubwa sana, wakati wengine wanaona hayo hayawezekani. Unafikiri ni kwa nini baadhi wanaweza kufanya makubwa huku wengine wakishangaa.

Nakumbuka kwenye kitabu cha THINK AND GROW RICH, kuna hadithi moja ya Hendry Ford aliyekuwa anamiliki kiwanda cha magari, aliwaita mainjinia wake na kuwaambia nataka mtengeneze gari ya injini yenye silinda nane. Mainjinia wake walimwambia hicho kitu hakiwezekani. Akawaambie nendeni mkafanye. Baada ya muda wakarudi kwake, wakamwambia tumejaribu sana, lakini kama tulivyokuambia, kwa sheria zote za kifizikia, injini yenye silinda nane ni kitu kisichowezekana kabisa. Ford aliwaangalia akawaambia naona hatuelewani, nimewaambia nataka injini ya kuingia silinda nane, na naitaka injini hiyo au mtakuwa hamna kazi. Walienda na kutengeneza injini hiyo.  Na kama umewahi kusikia watu wakisema gari aina ya V8 basi ndiyo hizo gari zenye silinda nane kwenye injini, zinakuwa na nguvu ya ziada ukilinganisha na magari mengine.

Unafikiri ni kitu gani kilikuwa kinampa Ford nguvu ya kuwaeleza mainjinia wake watengeneze injini hiyo? Yeye hakuwa na elimu kubwa kwenye mambo ya fizikia, lakini alijua kitu kimoja, kama anajua anaweza kitu basi anaweza. Na hakuwa na wasiwasi wowote.

Hichi ndiyo kitu unapaswa kuwa nacho rafiki yangu ili ufanikiwe, utaweza kama utajua ya kwamba unaweza na usiwe na shaka yoyote. Hata ukishindwa, haimaanishi kwamba huwezi, bali ulikuwa hujajua njia sahihi.

Jiambie sasa, na kila siku unapoamka kauli hii; NAWEZA KWA SABABU NAJUA NAWEZA. Kisha nenda kafanyie kazi kile unachotaka kufanikiwa. Kama hutatetereka, hakuna kinachoweza kukuzuia usifanikiwe.

Rafiki, nikutakie kila la kheri kwenye kuanza juma namba 33 la mwaka huu 2018. Usisahau kutenga muda wa kupangilia juma hilo kabla hujalianza, anza kufanya tahajudi kila siku na jiambie unaweza kwa sababu unajua unaweza.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji