Karibu kila dini na falsafa ina mafundisho yanayotukumbusha kwamba tulikuja duniani tukiwa watupu na tutaondoka tukiwa watupu. Chochote tunachotafuta na hata tukijiambia tunamiliki hapa duniani, hatutaondoka nacho.

Watu wanapata mali na wanazipoteza, watu wanakuwa na fedha nyingi na zinapotea. Na kwenye falsafa ya ustoa hatusemi umepoteza, bali umerudisha. Kwa sababu hakuna chochote ambacho unamiliki, bali umekopeshwa tu kwa muda.

Sasa mafunzo haya yote ni mazuri sana, kwa sababu yanatufanya tukumbuke jukumu letu hapa duniani, ambalo ni kutoa mchango wetu kwa wengine. Tusiishie kujishikiza na vitu ambavyo baada ya sisi kuondoka havitakuwa na maana tena.

Badala yake tuweke juhudi kwenye kuwahudumia wengine, ili hata tunapoondoka, tuache alama kwenye maisha ya wengine. Hichi ni kitu ambacho kila mmoja wetu anaweza kufanya, bila ya kujali yupo kwenye ngazi gani.

Huhitaji kuwa raisi wa nchi ndiyo uweze kuacha alama kwenye maisha ya wengine, wala huhitaji kuwa kiongozi wa dini au mwanafalsafa mkubwa ndiyo wengine wakukumbuke maisha yao yote.

Bali unaweza kuacha alama kwa kuchagua kufanya kile unachofanya sasa kwa namna ambayo utagusa maisha ya wengine.

Unaweza kuanzia hili kwenye ngazi ya chini kabisa, ngazi ya familia, ukawalea watoto wako kwa namna ambayo utawajenga vizuri kwa maisha ya baadaye. Wazazi wengine wakaona na wao wakalea watoto wao vizuri. Watoto waliopata malezi hayo bora nao wakatoa malezi bora kwa watoto wao. Na kwa njia hiyo, jamii ikawa bora sana.

Unaweza kufanya hili kwenye taaluma yako, kama ni mwalimu, daktari, mwanasheria, mhasibu na kadhalika, ukatoa huduma bora sana kwa wale wenye uhitaji wa huduma unayotoa. Kiasi kwamba maisha yao yanabadilika kabisa na wewe unakuwa ndiyo kichocheo.

Na hakuna sehemu nzuri ya kufanya hili kama kwenye biashara, kwa sababu hapa unachagua kuwahudumia wateja wako vizuri, kwa namna ambayo utayaboresha zaidi maisha yao na wao wataendelea kuwa na wewe.

Kupata ukuu kwenye maisha yako, unahitaji kutoa huduma kubwa kwa wengine. Na hilo lipo ndani ya uwezo wa kila mmoja wetu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha