Ni jambo la kushangaza lakini watu ambao hawajawahi kufanya biashara yoyote kwenye maisha yao wanaweza kugeuka kuwa washauri kwenye biashara yako.

Wengi huamini kwa sababu wanaona biashara nyingi, basi wana mengi ya kushauri kwa biashara yoyote ile.

Ni kweli kwamba kila mtu anaweza kuwa na ushauri mzuri kwenye aina yoyote ile ya biashara. Lakini ushauri ni kitu kimoja, kufanyia kazi ushauri huo ni kitu kingine ambacho ni kigumu zaidi.

Hivyo sisemi usisikilize ushauri wa yeyote, bali kuwa makini kabla hujaanza kufanyia kazi ushauri wowote unaopewa, hasa na wale ambao hawajawahi kufanya biashara yoyote.

Kumbuka anayekushauri anaongea na kuondoka, lakini wewe ndiye utakayebaki na biashara yako wakati wote, wewe ndiye utakayebeba mzigo wa mabadiliko unayoanzisha kwenye biashara yako.

Pia kumbuka wewe ndiye mwenye maono makubwa na biashara yako. Watu wanachoona kwa nje ni tofauti na unachoona kwa ndani. Hivyo pima kwa umakini kila unachopokea kama ushauri kabla hujafanyia kazi.

Na mara zote, kazana kuwa bora zaidi kwenye biashara yako, kulingana na maono makubwa uliyonayo kwenye biashara hiyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha