Rafiki yangu mpendwa,

Ili kuweza kufikia mafanikio makubwa, mabadiliko ni lazima. Watu wengi wanapenda sana kusema kuhusu mabadiliko, lakini pale wanapohitajika kubadilika wao wenyewe, huwa hawapo tayari kuchukua hatua.

Hii ni kwa sababu mabadiliko ni magumu na mabadiliko yana changamoto zake ambazo kubwa ni kutokuwa na uhakika. Watu huwa wanaona ni bora waendelee na kile ambacho wana uhakika nacho hata kama siyo bora, kuliko kujaribu kipya ambacho hawana uhakika nacho.

Changamoto nyingine kwenye mabadiliko imekuwa njia za mkato. Watu wanapogundua kwamba wanapaswa kubadilika, badala ya kuchukua hatua sahihi, wanakimbilia njia za mkato. Na njia hizo huleta matokeo mazuri, lakini yamekuwa hayadumu.

Kwa mfano mtu ambaye amekuwa na uzito mkubwa kuliko anaopaswa kuwa nao. Ili kuondokana na uzito huo, anahitaji kufanya mabadiliko makubwa kwenye maisha yake, kuanzia ulaji mpaka ufanyaji wa mazoezi. Sasa kwa kuwa wengi hawapendi kubadili maisha yao, wanatafuta njia ya mkato. Hapo ndipo mtu atatafuta dawa anayoambiwa inapunguza uzito, anaitumia, uzito unapungua kweli, lakini baada ya muda, uzito huo unarudi tena. Tatizo ni kwamba mtu anakuwa hajachagua kubadilika.

Mfano mwingine mzuri ni kwenye fedha. Mtu kipato chake hakitoshelezi, na maisha ni magumu. Badala ya kufanya mabadiliko makubwa kwenye maisha yake, yatakayomwezesha kuongeza kipato chake, anakimbilia kukopa. Ni kweli mkopo unamtatulia mahitaji yake aliyonayo sasa, lakini baadaye anabaki na shida yake ya fedha na mkopo juu.

NUFAIKA NA MABADILIKO

Rafiki yangu, yote haya ni kutaka kukuambia kwamba, kama kweli umejitoa kufanikiwa, basi njia za mkato na kukwepa mabadiliko havitakusaidia kabisa. Ni lazima uwe tayari kuweka kazi, lazima uwe tayari kubadilika na lazima uwe na uvumilivu ili kuweza kuyaboresha maisha yako.

Ili kuweza kufanya mabadiliko yatakayodumu kwenye maisha yako na kukuletea mafanikio makubwa, tumia njia hizi nne;

Njia Ya Kwanza; Jijue Wewe Mwenyewe.

Wanasema hatua ya kwanza ya kutatua tatizo ni kujua kwamba kuna tatizo. Hivyo kabla hujaanza kufanyia kazi mabadiliko, unahitaji kujijua wewe mwenyewe. Jua wapi upo sasa na wapi unakwenda, pia nini kinakuzuia kufika pale unapotaka kufika.

Jua ni maeneo gani unapaswa kulalamika na muhimu zaidi jua njia sahihi ya mabadiliko na kupata matokeo unayotaka kupata. Achana kabisa na njia za mkato kwa sababu hazitakupa matokeo mazuri.

Njia Ya Pili; Kuwa Na Nidhamu Binafsi.

Unaweza kuwa na hamasa kubwa ya kuanza chochote kile, lakini tunawajua wengi ambao huwa wanaanza vitu na hawavimalizi. Hii ni kwa sababu wanakosa kitu cha kuwafanya waendelee kufanya hata pale hamasa inaposhuka.

Hapa unahitaji sana kuwa na nidhamu binafsi. Nidhamu binafsi ni pale unapofanya kile ulichopanga kufanya, hata kama una kila sababu za kuacha kufanya. Utakapoanga kuchukua hatua, kutakuja kila aina ya sababu kwa nini usifanye kile unachopanga kufanya.

Unapokuwa na nidhamu binafsi, unaweza kufanya chochote unachopanga kufanya bila ya kuacha. Nidhamu binafsi ndiyo itakayokuvusha kwenye ugumu utakaokutana nao kwenye safari yako ya mabadiliko. Pia nidhamu binafsi itakuepusha usikimbizane na njia za mkato.

Panga nini utafanya na anza kufanya, endelea kufanya mpaka unapokamilisha, hata kama una sababu nyingi za kutokufanya.

SOMA; Chanzo Kikubwa Cha Mabadiliko Ya Maisha Yako, Kinaanzia Hapa.

Njia Ya Tatu; Chelewesha Raha.

Wanasema raha ni adui wa furaha. Raha ni yale matokeo ambayo yanapatikana kwa muda mfupi, lakini yanakuzuia kupata matokeo ya muda mrefu.

Ili kuweza kuleta mabadiliko kwenye maisha yako, unahitaji kuweza kuchelewesha raha. Wakati utakapoanza kufanyia kazi mabadiliko kwenye maisha yako, utakutana na maumivu. Na wakati huo huo kutakuwa na njia mbadala ambayo haina maumivu na ina raha.

Sasa kama hutaweza kuchelewesha raha, ukaikimbilia, utaondoka kwenye njia sahihi ya mabadiliko na kwenda kwenye njia isiyo sahihi. Usiyumbishwe na raha za muda mfupi, fanyia kazi furaha ya muda mrefu utakayoipata baada ya kuwa umekamilisha mabadiliko unayofanyia kazi.

Njia Ya Nne; Weka Kazi Hasa.

Watu wamekuwa wanajidanganya sana kuhusu kazi. Watu wamekuwa wakijiambia hawahitaji kuweka kazi sana, bali wanahitaji kutumia akili zaidi, na kinachotokea ni kutafuta njia za mkato ambazo zinawapoteza zaidi ya kuwasaidia.

Unapotaka kufanya mabadiliko kwenye maisha yako, lazima uweke kazi kubwa, lazima ufanye kazi kwa juhudi kubwa sana. Kwa sababu mabadiliko hayaji kirahisi, kazi lazima ihusike.

Kama haupo tayari kuweka kazi, utasumbuka na njia nyingi za mkato, ambazo mwisho wa siku hazitakufikisha kule unakotaka kufika. Jitoe kuweka kazi kubwa na ya maana ili kuweza kukamilisha mabadiliko na kupata unachotaka.

Tumia njia hizi nne kutengeneza mabadiliko ya kudumu kwenye maisha yako ili uweze kuwa na maisha ya mafanikio. Mara zote kumbuka, njia za mkato zitakuacha na mikato mingi kwenye maisha yako. Jua njia sahihi na itumie, itakupa matokeo sahihi.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha