Siku mpya,
Siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari MUDA UTASHINDA…
Hakuna jambo lolote hapa duniani ambalo limewahi kuushinda muda,
Hakuna kitu chochote kile ambacho hakijawahi kuguswa na muda.
Kwenye kila kitu, muda unabaki kuwa mshindi wa mwisho, hata kama ni kwa kuchelewa.
Hivyo mwanamafanikio, mara zote kaa upande wa muda, maana muda lazima ushinde.
Hata kama kile unachofanya kinaonekana ni kigumu kiasi gani,
Hata kama unaona umekutana na vikwazo vikubwa kiasi gani,
Hata kama unaona huwezi kuendelea tena kwa namna yoyote ile,
Wewe endelea, endelea kuwepo hapo, endelea kung’ang’ana na mwisho wa siku, muda utashinda na wewe utakuwa umeshinda.
Wale wanaofanikiwa zaidi kuliko wewe siyo kwamba wana akili sana kukushinda, au ni wajanja sana, wengi wanakaa upande wa muda.
Utawaona wakiendelea kupambana hata pale mambo yanapoonekana ni magumu.
Utawaona wakiendelea kuwepo licha ya wengine kukata tamaa.
Na kwa ung’ang’anizi wao, wanapata kile wanachotaka.
Wakati mwingine ni kama dunia inawajaribu watu, kutaka kuona nani anaweza kuvumilia zaidi ndiyo apewe kile anachotaka.
Hivyo mwanamafanikio, inapokuja kwenye ndoto yako kubwa, kaa upande wa muda na usikubali chochote kikuondoe kwenye kuendelea kuifanyia kazi ndoto yako.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kukaa upande wa muda.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha