Watu huwa wanasema kuna siku kubwa tatu kwenye maisha ya mtu, siku ya kuzaliwa, siku ya kuoa au kuolewa na siku ya kufa.
Kwa uelewa wa kawaida, hizi ndiyo siku kubwa zinazobadili kabisa maisha ya mtu yeyote yule.
Lakini kwa upande wa maisha ya mafanikio, kila siku ambayo mtu anaishi, ni siku kubwa, muhimu na ya kipekee sana kwake.
Kwa sababu hapo ulipo leo, ni matokeo ya siku uliyoishi jana, na jinsi utakavyoishi leo, ndivyo unavyoitengeneza kesho yako.
Kwenye siku yako yoyote ile, unaweza kuchukua hatua ambazo zitabadili kabisa maisha yako. Hatua ambazo zitakuwezesha kufanikiwa zaidi au kushindwa zaidi.
Ndiyo maana maisha yako yote ni mabadiliko, kila siku unayoishi ni siku ya mabadiliko, tangu unazaliwa mpaka siku unakufa.
Hii ina maana kwamba, kila wakati unahitaji kuwa tayari kwa mabadiliko, kila siku unahitaji kuwa tayari kuchukua hatua kubwa na bora zaidi ya ulivyozoea kuchukua.
Kama maisha ni safari, umuhimu haupo mwisho wa safari, bali umuhimu upo kwenye safari yenyewe.
Hivyo usisubirishe chochote kwa sababu unategemea mwisho uwe wa aina fulani, badala yake chukua hatua kwenye kila siku unayokuwa hai, na utaweza kupiga hatua zaidi.
Kila siku ni siku muhimu kwako, kila siku inapaswa kuwa sikukuu kwako, kila siku inapaswa kuwa siku unayoifurahia na kuchukua hatua kubwa.
Maisha yako yote, tangu unazaliwa mpaka siku utakayokufa, yatakuwa mwendelezo wa mabadiliko, kuwa tayari kubadilika na kuwa tayari kuwa bora zaidi na maisha yatakuwa mazuri sana kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,