“When I get a little money I buy books; and if any is left I buy food and clothes.” – Erasmus, 16th century scholar.

Hii ndiyo siku bora kabisa ambayo wote tulikuwa tunaisubiria.
Ni siku ya kipekee kupata kuwepo hapa duniani, kwa sababu ndiyo siku tunayoweza kuchukua hatua na kuyafanya maisha yetu kuwa bora zaidi.
Jana ilikuwa na yake, lakini imeshapita, kesho itakuja na yake, lakini bado hatujaifikia.
Lakini leo, LEO HII, tuna muda bora kwetu kwenda kuweka kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari NIONESHE UNANUNUA NINI KWANZA NA NITAKUAMBIA UTAFIKA WAPI NA MAISHA YAKO….

Watu wamekuwa wanatoa sababu kwamba hawanunui vitabu kwa sababu hawana fedha za kufanya hivyo, au vinauzwa ghali.
Lakini huwezi kukutana na mtu anatembea uchi, au amekufa na njaa kwenye zama hizi.
Kwa hiyo shida siyo fedha, bali shida ni vipaumbele.

Kama Erasmus anavyotuambia, kama ukipata fedha unaanza kununua vitabu kwanza, na kama iyabaki ndiyo ununue chakula na nguo, huwezi kamwe kukosa vitabu vya kusoma, na bado utakula na kuvaa.

Ninasema nioneshe unanunua nini kwanza na nitakuambia utakuwa wapi.
Kwa sababu kama hununui vitabu, kama hulipii kupata maarifa mbalimbali, huna unapokwenda.
Utakuwa unazunguka tu mduara, unarudi ulipoanzia na kuanza tena.

Kama unanunua chakula lakini hununui maarifa, utashiba na mwili utakuwa na afya, lakini utakuwa na utapiamlo wa akili, kitu ambacho kitakuwa mzigo kwako pale unapotaka kufanikiwa.
Kwa sababu nisikudanganye, kama una utapiamlo wa akili, yaani akili yako haina maarifa ya kutosha, safari ya mafanikio itakuwa mateso makubwa sana kwako. Mafanikio yanahitaji akilo yenye afya sana, inayoshibishwa maarifa kila wakati.

Kama unanunua nguo lakini hununui maarifa, utasitiri mwili lakini akili unaiacha uchi.
Na hakuna kitu kinacholeta aibu kama akili iliyo uchi.
Hivi umewahi kuwa mahali na mtu ambaye amevaa vizuri kabisa, na kila mtu anamwona mtu huyo ni wa maana. Lakini anapofungua mdomo kuongea kila mtu anaangalia pembeni? Na wengine inabidi wabadili mazungumzo kumsitiri mtu huyo?
Najua umeshaona hayo mara nyingi, na huenda imeshatokea kwako pia. Hapo mwili ulikuwa umevaa, lakini akili ilikuwa uchi kabisa.

Rafiki, ukipata fedha, cha kwanza kununua ni maarifa, halafu inayobaki unanunua chakula na mavazi.
Fanya kinyume chake na utatembea na akili yenye utapiamlo na iliyo uchi, na hakuna kikubwa utafanya na maisha hako.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kupata na kulisha akili yako maarifa sahihi ili iwe imara na isitirike.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha