Wale wanaosema kwamba mafanikio au fedha hazileti furaha, kuna kitu wanakuwa hawajakielewa tangu mwanzo wa safari.
Furaha kwenye maisha siyo mwisho wa safari, bali ni safari yenyewe. Usifikiri kwamba kama unaanzia chini, huna kitu basi ukishapata unachotaka utakuwa na furaha sana.
Kwa sababu kwenye kupata hakuna mwisho, na hakupaswi kuwa na mwisho.
Kama unatembea kwa miguu utasema ukipata baiskeli itakuwa rahisi ziadi kwako. Ukipata baiskeli, kuchochea kunakuchosha na unagundua huwezi kubeba mzigo mkubwa, unaanza kufikiria kupata pikipiki. Ukipata pikipiki unagundua siyo salama sana kwa afya yako, na huwezi kubeba familia yako yote, unafikiria kupata gari.
Sasa kama lengo lako ni kuwa na furaha kwa kupata unachotaka, utagundua kila unachopata, kinakufanya uone unahitaji kupata zaidi. Kwa hiyo kama furaha umeiweka kwenye kupata, hutafikia furaha kwa sababu kila unapopata kile unachoendea, ndiyo unaona vingi zaidi unavyoweza kupata.
Maisha yako hivi, kwenye ngazi uliyopo sasa, unaona ngazi moja mbele yako. Unaweza kufikiri hiyo ndiyo ngazi pekee uliyobakiza. Lakini ukishapanda kwenye ngazi hiyo, utaona ngazi nyingine zaidi mbele yako. Ukijishawishi umebakiza hiyo tu, ipande na utashangaa ngazi nyingine tena mbele yako imejitokeza.
Sasa lengo siyo kuzimaliza ngazi, huwezi, hakuna ambaye amewahi kuzimaliza ngazi zote. Lengo ni kupanda ngazi nyingi uwezavyo. Kadiri ulivyo hai, basi kazana kupanda ngazi nyingi uwezavyo. Na hupandi kwa sababu unataka kuzimaliza ngazi, au kwamba ukishapanda basi utapata furaha. Bali unapanda ngazi zaidi kwa sababu ni sehemu ya maisha, kwa sababu ndiyo njia pekee ya kuishi maisha yako.
Endelea kupanda ngazi zaidi kwenye maisha yako na usifike mahali ukajiambia umemaliza ngazi zote. Kila ngazi unayopanda inakuwa na changamoto fulani, ukitatua changamoto hiyo unapata nafasi ya kupanda kwenda ngazi ya juu zaidi.
Ishi maisha yako kwa kupiga hatua zaidi, panda ngazi zaidi na kuwa bora zaidi kila siku. Usiamke siku yoyote na kujiambia nimemaliza ngazi zote, nimefika kileleni, kwani siku hiyo ndiyo utaanza kuanguka.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,