Kipimo cha wengi kwenye ukuaji wa biashara kimekuwa ni idadi ya wateja wanaokuja kwenye biashara hiyo.

Hivyo mfanyabiashara anapoona wateja wanaokuja ni wengi, anaona biashara unakuwa na ina mafanikio makubwa.

Na hili ndiyo linalopelekea wafanyabiashara wengi kushusha bei ya bidhaa au huduma zao, ili kuvutia wateja wengi zaidi. Kwa sababu wanaamini wateja wakiwa wengi basi biashara imefanikiwa.

Lakini zipo biashara zenye wateja wengi na hazina mafanikio makubwa, hazikui na wateja hao wanakuwa siyo wa kudumu.

Kipimo sahihi kabisa kwenye ukuaji wa biashara yako siyo idadi ya wateja wanaokuja, bali ubora wa huduma unayotoa kwa wateja wako.

Je wateja wanapata huduma ambayo hawawezi kuipata sehemu nyingine yoyote? Je wateja wanapotoka kwenye biashara yako wapo tayari kumwambia kila mtu aje kwako na apate kile kizuri ambacho amepata yeye?

Kwa sababu kama wateja hawajafikia hatua hiyo ya kuwa mashabiki na wapenzi wa biashara yako, bado biashara yako haijafanikiwa.

Nimekuwa nakuambia mara kwa mara, lengo kuu la biashara ni kutengeneza wateja ambao watakuwa wanaiamini na kutegemea biashara yako. Kwa sababu ni rahisi kumuuzia mteja ambaye alishanunua tena kuliko kumuuzia mteja mpya.

Njia pekee ya kutengeneza wateja wa aina hii, ni kutoa huduma bora kabisa, huduma ambayo hawawezi kuipata sehemu nyingine yoyote ila kwako tu.

Kukazana kuwahudumia wateja wengi, na kuwahudumia hovyo kwa sababu unao wengi, siyo njia bora ya kuuza biashara yako. Bali kuwahudumia vizuri wateja ulionao, hasa wakiwa kiasi ambacho unaweza kuwahudumia vizuri, ni njia bora kabisa ya kukuza biashara yako.

Kazana kutoa huduma bora kabisa kwa wateja ulionao, na namba ya wateja unaohudumia itajijali yenyewe. Lakini ukiacha kutoa huduma bora na ukaanza kukimbizana na namba, utakosa namba na utakosa wateja pia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha