Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KAMA UNASHANGAZWA, HUJAJIANDAA…
Kuna mambo mengi ambayo yanatokea kwenye maisha yako, ambayo hukutegemea yatokee.
Unapanga hivi unapata vile.
Unategemea mambo yaende vizuri unakutana na changamoto na vikwazo.
Watu wanakuahidi watafanya vitu fulani, unapofika wakati wa kufanya wanakuja na sababu.

Kama unashangazwa na lolote kati ya hayo, ukweli ni kwamba unakuwa hujajiandaa.
Yaani kama kitu amnacho hukutegemea kitokee kinatokea, halafu wewe unashangaa, na kujiambia kwa nini wewe, unakuwa hujajiandaa kabisa.

Kwa sababu unapojiandaa unajua kabisa kwamba siyo kila kitu kitaenda kama ulivyotegemea kiende.
Unajua siyo kila aliyeahidi atafanya kama alivyoahidi.
Na hivyo unakuwa na njia mbadala, iwapo zile ulizopanga kutumia hazitawezekana.

Jiandae kwa kila unachopanga na kufanya ili kupunguza kushangazwa na yale yanayotokea.
Jua kupanga kwako ni kama mwongozo rahisi kwako, lakini siyo kila kitu kitaenda kama ulivyopanga, na hivyo unahitaji kuwa na hatua mbadala za kuchukua ili usikwamishwe na chochote kile.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa na maandalizi na njia mbadala ilo usikwame wala kushangazwa.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha