Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UTAHUKUMIWA…
Moja ya vitu ambavyo watu wanapenda sana ni kukubalika na kila mtu, kila mtu afurahie kile ambacho tunafanya.
Lakini hicho siyo kinachotokea.
Kila utakachofanya kwenye maisha yako, wapo watu watakaokuhukumu.
Wapo watakaosema unakosea,
Wapo watakaosema unafanya vibaya,
Na wapo watakaosema unafanya vizuri.
Hakuna namna unayoweza kuwafanya watu wote wawe na hukumi sawa juu yako.
Sasa je utamsikiliza nani kwenye maisha yako?
Yupo mtu mmoja pekee aliye sahihi, ambaye hukumu yake ndiyo inapaswa kukuongoza.
Mtu huyo ni wewe mwenyewe.
Angalia, wewe ndiye unayejua wapi unakwenda na maisha yako,
Wewe ndiye unayejua wapi unataka kufika,
Na wewe ndiye unayejua njia sahihi ya kukufikisha pale.
Unahitaji kufuata njia hiyo sahihi.
Ukianza kusumbuka na kila mtu anafanya au kutaka nini, hutaweza kupata kile unachotaka.
Maana watu wengi hawajui hata wanataka nini na maisha yao, ndiyo maana wana muda mwingi wa kuhukumu wengine.
Usiumizwe na hukumu za wengine juu yako, hakuna wanachojua kuhusu wewe na kule unakokwenda. Na pia hakuna pakubwa wanakokwenda wao wenyewe.
Je unakubali kubabaishwa na watu wasiojua wanapeleka wapi maisha yao?
Ukawe na siku bora sana ya leo, siki ya kuweka juhudi na kuachana na hukumu za wengine.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha