Kama maisha ni nyumba basi tunaweza kusema kitu kimoja, ni nyumba ambayo ujenzi wake haujakamilika, na kila siku kuna kitu kinaendelea kujengwa.
Wengi huwa tunachukulia maisha kama kuanza ukiwa hujakamilika, kisha kukamilika na maisha kuwa mazuri, pale unapokuwa umefanikiwa.
Lakini wale wanaofuata njia hiyo, huwa wanaishia kuanguka. Pale mtu anapofikiria kwamba ameshakamilika, ndiyo anapoanza kuanguka.
Ukweli kuhusu maisha ni kwamba hakuna ukamilifu. Kuna vitu vingi sana ambavyo bado huvijui. Na mpaka siku unayoingia kaburini, kuna vitu vingi utaondoka ukiwa hujavijua.
Hivyo lengo kuu la maisha yako linapaswa kuwa bora zaidi kila siku, unapoimaliza leo, uwe bora zaidi ya ulivyoianza siku hii.
Nimewahi kukuambia tena kwamba maisha ni sawa na kupanda ngazi, hivyo mafanikio siyo kufikia ngazi fulani na kisha kukaa hapo, bali kuendelea kupanda ngazi zaidi. Maana ngazi za maisha hazina mwisho.
Kwa kuelewa hili basi, usiahirishe furaha yako. Wale unaowasikia wakisema kwamba wamefanikiwa ila bado hawana furaha, jua walikosea sehemu moja. Walifikiri furaha inaletwa na mafanikio. Wakati furaha ni matokeo ya mchakato mzima, na siyo mwisho wa mchakato.
Furaha yako inapaswa kutokana na hatua unazopiga kila siku, na siyo kilele ambacho unakiangalia. Kwa sababu ukifika kwenye hicho kilele unachoona sasa, utaona kilele kingine kikubwa zaidi.
Maisha yako hayajakamilika na hayatakamilika kadiri unavyoendelea kuwa hai. Mambo yanabadilika na unahitaji kuwa bora zaidi kila siku. Pokea hili kwa furaha na weka juhudi zaidi kwenye mchakato kuliko kuangalia kilele fulani, maana ukifika kwenye kilele hicho, utaona kilele kingine.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,