Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUNA GHARAMA YA KULIPA…
Kila kitu unachochagua kufanya au kutokufanya kwenye maisha yako, kuna gharama unayolipa, iwe unajua au hujui.
Kila aina ya maisha unayochagua kuishi, kuna gharama ambayo lazima uilipe.
Hakuna maisha ya bure hapa duniani, kila kitu kina gharama na malipo yake.

Kuwa tajiri kunakutaka ulipe gharama kubwa kwenye kazi, muda, nguvu, uvumilivu na nidhamu. Lazima uwe tayari kuachana na vitu unavyopenda, lazima uwe tayari kuweka kazi na nguvu zaidi.

Kuwa masikini kunakutaka ulipe gharama ya uzembe, uvivu na kukata tamaa. Umasikini utakutaka ujione ni wa chini, ujione huthaminiwi, ujistukie kwambwa watu hawakuheshimu au kukusikiliza kwa sababu wewe ni masikini. Pia umasikini utakufanya ujione wewe ni mhanga wa kila kinachotokea na kuishia kuwalaumu wengine kwa kila kinachotokea kwenye maisha yako.

Hakuna utakachofanya kwenye maisha yako uache kulipa gharama.
Hivyo basi, kwa nini usichague kulipa gharama ya kupata kile unachotaka hasa, kile ambacho unaweza kujivunia kwa wengine. Kwamba hata kama kimekugharimu sana, ndicho hasa ulichotaka.

Kwenye kila unachochagua kufanya, kwenye maisha unayochagua, jiulize ni gharama ipi unayolipa na kama gharama hiyo inakupa kile hasa unachotaka.
Jitoe kulipa gharama ya kupata unachotaka, maana hata usipopata hicho, kuna gharama utalipa kupata vitu vingine.

Ukawe na siku bora sana ya leo,
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha