Watu hushangazwa sana pale wanapoona baadhi ya watu waliofanikiwa wakianguka. Wanawaona watu ambao wametoka chini, wamejitahidi na kupata mafanikio, lakini wanaanguka na kurudi chini kabisa.

Kinachotokea ni hiki; wengi wanapoanza wanaweka juhudi kubwa sana, wanajituma mno, hawachagui kazi, wanafanya kazi kwa muda wa ziada, wanakuwa tayari kuumia, wanakuwa wavumilivu hasa na wanapenda sana kile wanachofanya.

Kwa juhudi na mapenzi ya aina hiyo, matokeo mazuri yanaanza kuonekana, na yanaendelea kukaribisha matokeo mazuri zaidi na zaidi.

Sasa inafika hatua fulani, ambapo mtu anapozidi kufanikiwa, anapofikia kile alichokuwa anakitaka, anaanza kufikiria kwamba ameshamaliza kila alichokuwa anataka. Anaona kwa hatua aliyofikia, hahitaji tena kujisukuma kama mwanzo. Sasa anaweza kupumzika zaidi, anaweza kuacha kuweka juhudi kubwa, anaweza kuacha kuweka muda mwingi kwenye kazi.

Anachofikiria mtu ni kwamba, akishafanikiwa basi sheria zinabadilika. Yaani kama vile mtu amepanda cheo basi kazi zinabadilika.

Na hapo ndipo wengi wanapoanza kuanguka. Kwa sababu wanaacha kufanya kile wanachopenda na kilichowafikisha kwenye mafanikio.

Rafiki, kumbuka sheria hazibadiliki kwa sababu umefanikiwa, bali sheria ndiyo zimekufikisha kwenye mafanikio na zitakazokufanya ubaki kwenye mafanikio hayo. Siku utakapoacha sheria zako, ndiyo siku utakayoanguka kutoka kwenye mafanikio.

Kile unachofanya kila siku ndiyo unachopaswa kuendelea kufanya kwenye maisha yako. Kila siku unapaswa kufanya kama ndiyo siku ya kwanza. Weka juhudi kubwa, jitume, weka nguvu, weka muda na weka mapenzi yako kwenye kila unachofanya, na mafanikio yatadumu na wewe muda wote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha