Kwenye zama tunazoishi sasa, zama za taarifa, taarifa ni nyingi kuliko uwezo wa mtu yeyote kuzipata zote. Hivyo hili linawaweka wengi kwenye hofu ya kupitwa, kitu kinachowapelekea kupoteza muda mwingi kukimbizana na vitu ambavyo havina umuhimu mkubwa kwao.
Njia pekee ya kuondokana na hali hii ya kukimbizana na kila aina ya taarifa, wewe unahitaji kuwa habari, kuwa mwandishi wa habari, ambaye utazungumzia yale ambayo ni muhimu kwako, yale unayoyajali.
Unahitaji kuingia kwenye kelele hizi za wingi wa taarifa ukiwa na ujumbe ambao ni muhimu kwako, ukijua kabisa wapo wengine ambao watanufaika sana na ujumbe huo.
Hivyo kwa njia yoyote utakayoweza, iwe ni kuwa na blogu, kuandika kitabu, kutumia mitandao ya kijamii, washirikishe wengine kile unachoona ni muhimu, kile unachojifunza na uzoefu unaopata kadiri unavyokwenda na maisha yako.
Huwa nasema kila mtu ana kitabu ndani yake, kila mtu ana kitabu ambacho dunia haijawahi kusoma, na wapo watu wengi ambao wamekwama kwenye maisha yao, ambao kama wangesikia hadithi yako, wangepata tumaini la kuamka na kuendelea tena.
Wewe ndiye habari, wewe ndiye chombo cha habari, ongelea yale ambayo ni muhimu zaidi kwako na kuna watu watakaonufaika. Kama kuna aina ya habari hupendi, achana nazo.
Unaweza kutumia njia yoyote unayotaka na kuweza, tumia maandishi, tumia picha, tumia sauti tumia video, muhimu ni ujumbe ufike kwa wale unaowalenga.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,