Rafiki yangu mpendwa,

Hakuna kipindi rahisi kufanikiwa kwenye maisha kwa chochote kile ambacho mtu amechagua kufanya kama sasa.

Kwa sababu, licha ya kuonekana ushindani ni mkali na kila mtu anaweza kufanya kila kitu, bado huu ndiyo wakati bora kabisa wa kusimama na kujitofautisha kabisa na kila mtu.

Ukweli ni kwamba, watu 99 katika watu 100 ni wavivu, wazembe, wanaotafuta njia ya mkato ya kufanikiwa, wasiokuwa na msingi unaoendesha maisha yao na hawajui nini hasa wanataka kwenye maisha yao. Watu wote hawa, wanapoteza muda wao wa thamani, wakikimbizana na vitu ambavyo haviwezi kuwasaidia kabisa, kama kukimbiza njia za mkato za mafanikio.

Hii ina maana kwamba, kama wewe utachagua kuwa mmoja katika wale 100, ambaye unajituma na kuweka juhudi kubwa, unaweka umakini mkubwa kwenye kila unachofanya, upo tayari kutumia njia sahihi ya kufanikiwa na unajua nini hasa unachotaka na maisha yako, ni rahisi sana kwako kufanikiwa.

Njia ya uhakika ya kufanikiwa kwenye maisha yako, ni kutatua TATIZO GUMU na linalowasumbua wengi, ambalo wengi wanakwepa kulitatua, kwa sababu ni gumu na linahitaji siyo tu kazi ya nguvu, bali kazi ya hisia pia.

Ukijitoa kutatua tatizo la aina hiyo, na ukaweka juhudi zako zote kwenye kulitatua, utajitofautisha na wengine wote, na wakati huo pia utawafikia wale ambao wanataka sana tatizo walilonalo litatuliwe, na hivyo kuwa na nafasi nzuri ya kufanikiwa.

NUFAIKA NA MABADILIKO

Hivyo kuna sifa kuu mbili za aina ya tatizo unalohitaji kutafuta na kutatua ili kuweza kufanikiwa kwenye jambo lolote lile.

Sifa ya kwanza ni tatizo liwe gumu, na wengi wanalikwepa kwa sababu ya ugumu wake. Wewe unahitaji kuwa mtu wa kupenda vitu vigumu, kiasi kwamba watu wanaambiana kabisa, vitu vigumu fulani anaviweza. Usiwe mtu wa kukwepa na kukimbia matatizo fulani kama walivyo wengi. Unapoona tatizo ni gumu furahia, kwa sababu unajua siyo wengi watakaoliweza tatizo hilo.

Sifa ya pili ni tatizo liwe linawasumbua watu wengi na wanahangaika sana kulitatua. Tatizo linaweza kuwa gumu kweli kweli, lakini kama hakuna anayelijali, halina maana kwako kuhangaika kutatua. Unahitaji kuangalia kama watu wanajali sana kuhusu tatizo hilo, kama watu wanakosa usingizi, kama watu wapo tayari kutoa fedha ili tatizo hilo litatuliwe. Ukikutana na tatizo la aina hiyo, ambalo watu wameshachoshwa nalo na wapo tayari kulipia litatuliwe, umekutana na mgodi wa dhahabu, kazi ni kwako kuchimba.

SOMA; Piga Hatua Moja Kwa Wakati; Ushauri Muhimu Kwa Mafanikio Kwa Wanaoanzia Chini Kabisa.

Kumbuka tatizo gumu na ambalo watu wanataka sana kulitatua linaweza kuwa kwenye kila eneo la maisha. Ndiyo maana kwenye kila eneo la maisha kuna watu waliifanikiwa. Iwe ni kwenye afya, sheria, biashara, elimu na kadhalika. Wapo waliofanikiwa sana na wapo walioshindwa. Hivyo usijidanganye kwamba kama ungekuwa kwenye fani fulani au biashara fulani ndiyo ungefanikiwa. Popote ulipo, unaweza kufanikiwa kama tu utakuwa tayari kutatua tatizo gumu ambalo linawasumbua wengi.

Uwepo wetu hapa duniani ni kwa ajili ya wengine, na wengine wapo kwa ajili yetu. Maendeleo yote ya dunia yametokana na wale watu ambao walijitoa kutatua matatizo yaliyowaathiri wengi. Mfano kabla ya kuja kwa magari, watu walikuwa wanatumia punda na farasi kwa usafiri. Mtu aliona namna ilivyo mateso kutumia njia hizo za usafiri, na kuja na suluhisho, ambalo halikuwa rahisi.

Na hii ndiyo maana nakusihi sana rafiki yangu, tengeneza msingi wako kwenye kutatua matatizo ya wengine. Achana na uvivu, achana na kutafuta njia za mkato. Watu wanapokuja kwako na kukuambia wana fursa nzuri ya kutajirika haraka, swali la kwanza kuuliza liwe ni tatizo gani tunalotatua kwa wengine? Kama hakuna tatizo linalotatuliwa, na liwe tatizo halisi siyo la kuwajengea kwanza watu hofu ya tatizo, achana na fursa za aina hiyo.

Watu pekee ambao hawatakuja kukosa kitu cha kufanya hapa duniani, hata kama teknolojia itakua kiasi gani, ni wale ambao wanatatua matatizo ya wengine. Wengine wote watapotezwa, na watasumbuka sana na kutafuta njia za mkato, wasiambulie mafanikio yoyote.

Tafuta tatizo kubwa na gumu, linalowasumbua wengi na wapo tayari kulitatua, kisha weka maisha yako kwenye kutatua tatizo hilo, hakuna kitakachokuzuia wewe kufanikiwa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

Usomaji