Rafiki yangu mpendwa,

Kila mtu anapenda kulipwa zaidi, na hilo ni hitaji la yeyote anayejihusisha na shughuli yoyote ile ya kiuchumi.

Iwe mtu ameajiriwa, amejiajiri au anafanya biashara, hakuna asiyependa kupata fedha zaidi.

Lakini changamoto kubwa ni kwamba, wengi wanatumia njia ambazo haziwawezeshi wao kulipwa zaidi.

Kwa mfano, mtu ambaye ameajiriwa, njia kubwa anayotumia kutafuta kulipwa zaidi ni kuomba ongezeko la mshahara na kama asipopata basi anaweza kugoma au kuandamana akidai haki yake.

Na kwenye biashara, wengi wanaotaka kupata faida zaidi wanakimbilia kufanya vitu ambavyo baadaye vinawaumiza. Mfano wengi hupunguza bei ili kupata wateja zaidi, kitu ambacho kinaweza kuongeza kipato kwa muda mfupi, lakini baadaye kinakuwa mzigo zaidi kwao. Wengine wanaongeza tu bei bila ya kuongeza thamani. Na wengine wanakazana kupiga kelele zaidi ili kupata wateja zaidi.

Njia zote hizo rafiki, kuanzia kwenye kuajiriwa mpaka kwenye biashara, siyo sahihi.

Leo nakwenda kukushirikisha njia sahihi ya kuongeza thamani ya kile unachofanya ili uweze kulipwa zaidi kadiri unavyotaka wewe mwenyewe.

cropped-mimi-ni-mshindi

Na ili kujua njia hii, lazima kwanza tujue msingi mkuu unaoendesha uchumi. Kipindi cha mavuno, mazao huwa yanauzwa kwa bei rahisi sana, lakini kipindi ambacho siyo cha mavuno, mazao yanakuwa na bei ghali. Kadhalika, chuma na dhahabu vyote ni madini, lakini chuma ni bei rahisi kwa sababu inapatikana kirahisi, na dhahabu ni bei ghali kwa sababu inapatikana kwa ugumu.

Kanuni kuu inayoendesha uchumi ni UPATIKANAJI NA UHITAJI, au kama wanavyoita kwa kiingereza, SUPPLY AND DEMAND. Kama kitu kinahitajika sana, lakini upatikanaji wake unakuwa mgumu, bei ya kitu hicho inakwenda juu. Kwa sababu watu wanakitaka kweli na hawawezi kukipata, hivyo kile kinachopatikana, kinakuwa na thamani kubwa. Lakini kama kitu kinapatikana kwa wingi, bei yake inakuwa chini kwa sababu kila mtu anaweza kupata atakavyo.

SOMA; Njia Ya Uhakika Ya Kufanikiwa Ni Kutatua Tatizo La Aina Hii. Lijue Na Chukua Hatua Sasa.

Kwa kutumia kanuni hiyo muhimu inayoendesha uchumi, unaweza kuongeza sana thamani yako na ya kile unachofanya, kwa kutoa kitu ambacho wengine hawawezi kukipata sehemu nyingine yoyote bali kwako. Unahitaji kuhakikisha upatikanaji wa unachotoa ni mgumu kwa wengine, na rahisi kwako, hivyo watu wanakutegemea wewe kwa kile unachofanya.

Kama umeajiriwa, unahitaji kufanya kazi yako kwa upekee wa hali ya juu sana kiasi kwamba mwajiri wako hawezi kupata mtu mwingine wa kufanya kazi kama unavyofanya wewe.  Na ukishafikia ngazi hizo, yeye mwenyewe atakuongeza kipato kabla hata hujaomba, kwa sababu hatataka kukupoteza. Kama kweli unamtengenezea mwajiri wako thamani ambayo hawezi kuipata kwa mwingine yeyote, hatasita kukulipa zaidi ili aendelee kunufaika na thamani hiyo.

Kwenye biashara, unahitaji kutoa huduma tofauti kabisa na wanayotoa wafanyabiashara wengine. Wateja wanahitaji kujua huduma fulani ambayo ni bora zaidi inapatikana kwako tu na siyo kwa wafanyabiashara wengine. Kwa njia hii, unaweza kuuza kwa bei ya juu kuliko wengine na bado wateja wakafurahia kupata kile unachotoa.

Wengi wanaposikia hii ndiyo njia ya kuongeza thamani kwenye kile wanachofanya, wanajiambia haiwezekani, kwa sababu wanaona hakuna cha tofauti wanachoweza kufanya. Na hawa ndiyo watu wavivu wa kufikiri na kuchukua hatua, ambao wanafanya kila kitu kwa mazoea mpaka wameshaona mazoea ndiyo sehemu ya maisha.

Haijalishi unafanya nini, una uwezo wa kufanya kitu cha tofauti, una uwezo wa kufanya kile ambacho hakuna mwingine anayeweza kufanya. Kwa sababu dunia haijawahi kupata mtu kama wewe. Jiweke wewe kwenye kila unachofanya, na kwa hakika utaleta utofauti wa hali ya juu sana.

Dunia inataka wewe uwe sawa na wengine ili ikupe kile ambacho kila mtu anapata. Kama unataka kufanikiwa zaidi, lazima uende kinyume na dunia inavyotaka uwe, lazima uwe wewe na lazima utoe kile kilichopo ndani yako.

Ongeza thamani ya unachofanya kwa kutoa vitu adimu, vitu ambavyo havipatikani kwa wengine bali kwako tu, kwa njia hii, watu watakuwa tayari kukulipa zaidi.

Usijidanganye, hili linahitaji kazi, linahitaji kujituma, linahitaji uvumilivu, linahitaji muda na linahitaji kujitoa zaidi ya kawaida. Fanya hivyo na utaweza kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

Usomaji