Hongera mwanamafanikio kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ambayo tumeipata leo.
Ni nafasi nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa na kupata matokeo bora kabisa.
Orodhesha yote unayokwenda kufanya leo, na hakikisha unafanya kweli.
Usiruhusu kujiambia utafanya kesho, maana hakuna kesho, leo ndiyo muhimu kwako.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari RUDIA RUDIA…
Kinachokusaidia kwenye maisha yako, siyo kile unachojua, bali kile unachorudia rudia mara nyingi.
Watu wengi ambao hawapigi hatua kwenye maisha yao, tayari wanajua kila kitu. Lakini vile wanavyojua haviwasaidii, kwa sababu kujua mara moja hakusaidii, ni kurudia rudia ndiyo kwenye msaada.
Mfuate mtu ambaye ni masikini, hana fedha, mpe kitabu ambacho kina maarifa ya kuondoka kwenye umsikini, atakuambia nayajua yote hayo. Sasa utashangaa kama anayajua kwa nini bado yupo kwenye umasikini?
Kwa sababu ni kweli anaweza kuwa anajua kila msingi wa kuondoka kwenye umasikini; KUFANYA KAZI KWA BIDII, KUPUNGUZA MATUMIZI, KUONGEZA KIPATO, KUWEKA AKIBA NA KUWEKEZA.
Lakini kwa kuwa harudii rudii mpaka ikawa kama sala kwake, anajikuta anarudia makosa ambayo angepaswa kuyaepuka.
Hivyo rafiki, kamwe usijiambie tayari unajua chochote kile, kuwa mpole na jifunze tena. Kinachokusaidia siyo unachojua, bali unachorudia rudia kwenye maisha yako.
Unaporudia kitu kuna kipya unajifunza, unaona suluhisho la changamoto unazokutana nazo.
Maisha ni kurudia rudia, iwe ni kweye kujifunza, kwenye kazi, kwenye biashara.
Hakuna utakachofanya mara moja kikakupa kila unachotaka.
Unavyorudia rudia ndiyo unaimarisha kile unafanya na kupata matokeo bora.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kurudia vile ambavyo unajiambia tayari unajua au umeshafanya.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha