Mtoto mdogo anaweza kufanya chochote anachotaka kufanya, bila ya kuwa na hofu au kufikiria matokeo yatakuwaje. Hii ni kwa sababu mtoto huyo anakuwa hana ufahamu na utambuzi wa kina juu ya kile anachofanya.
Kadhalika mpumbavu anaweza kufanya kitu ambacho wengine wanabaki midomo wazi lakini yeye hana wasiwasi. Hiyo ni kwa sababu hana ufahamu na utambuzi juu ya kile anachofanya.
Kila kitu kwenye maisha kinakuja na gharama zake, hata kile kinachotusaidia sana, kinakuja na madhara au hasara zake.
Ufahamu na utambuzi unatusaidia kuweza kuchukua hatua sahihi kwenye maisha yetu, lakini pia kunakuja na gharama ya kutupa hofu.
Pale unapojua matokeo mabaya yanayoweza kutokea, unaogopa kuchukua hatua kwa kuogopa kupoteza. Hapo unasahau ya kwamba matokeo mazuri pia yanaweza kutokea na unaegemea kwenye matokeo mabaya pekee.
Kila unapopanga kuchukua hatua kubwa, lakini unapatwa na hofu, jua hiyo ni gharama ya kuwa na ufahamu na utambuzi. Maana usingekuwa na ufahamu wa kutosha, usingekuwa na hofu kabisa, ungeenda tu kama mtoto.
Lakini sasa, usikubali hofu unayopata ikuzuie kwa namna yoyote ile, badala yake, pokea hofu kama sehemu ya ufahamu wako, kisha chukua hatua ukijua njia ipi bora ya kupata kile unachotaka.
Pia jikumbushe, kila kitu kina pande mbili, upande mzuri na upande mbaya. Hivyo usiishie kuangalia upande mbaya pekee, badala yake angalia na upande mzuri pia, ambao unaweza kutokea pia.
Kuwa na ufahamu na utambuzi, ni kitu kizuri kwetu, lakini tusipojua hatari zake, tutaishia kuwa watumwa wa ufahamu wetu na kushindwa kuchukua hatua kubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,