Moja ya vitu muhimu sana unavyopaswa kujua ni kwamba, kuuza ni kuwa na msimamo.

Kama huna msimamo huwezi kufanikiwa kwenye mauzo. Utauza kwa kadiri utakavyokuwa na msimamo.

Kwa sababu mara ya kwanza utakapowaambia watu kitu hawatachukua hatua, mara ya pili pia hawatachukua hatua, utakwenda mpaka mara ya sita, ndiyo wengi wataanza kuchukua hatua.

Sasa kama unataka uwaambie watu kitu mara moja na wachukue hatua hapo hapo, unajidanganya.

Kuuza ni msimamo, na msimamo unaanza kwa kufanya kilicho bora wakati wote bila ya kuyumba au kurudi nyuma. Na pia msimamo unahusisha kuwaambia watu kila wakati bila ya kuchoka kuhusu unachouza na jinsi kinavyoweza kuwasaidia.

Watu wengi unaowaambia kwa mara ya kwanza hawatakuwa na imani sana kuhusu wewe, hivyo watasubiri, wakiona bado upo na unaendelea kuwaambia, wanashawishika kuja kujaribu.

Tatizo kwa wafanyabiashara wengi, wanaanzisha huduma fulani, mwanzoni wanaona hakuna wateja, wanaachana nayo. Kumbe kuna watu walishawasikia, ila wanasubiri waone kama wataendelea kuwasikia zaidi kabla hawajatoa fedha zao.

Kuuza ni msimamo, kuwa na msimamo na utauza zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha