“What lies in our power to do, lies in our power not to do.” — Aristotle

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UNACHOWEZA KUFANYA, UNAWEZA KUTOKUFANYA…
Kila unachochagua kufanya wewe mwenyewe, jua pia unayo nguvu ya kuchagua kutokufanya.
Kila kilicho ndani ya uwezo wetu wa kukifanya, kipo pia ndani ya uwezo wetu kutokukifanya.

Na hili linaweza kutusaidia kwa pande mbili:
Upande wa kwanza ni kuachana na tabia ambazo siyo nzuri kwetu. Wengi huona hawana namna ya kuondokana na tabia hizo, lakini nguvu ipo ndani ya kila mtu, kama anavyoweza kufanya, ndivyo pia anavyoweza kutokufanya.
Hivyo usijidanganye kwamba huwezi kubadili tabia fulani ulizonazo, nguvu ipo ndani yako, ni wewe tu kuchukua hatua.

Upande wa pili ni kuepuka kuacha kufanya.
Watu wengi wanapoanza kufanya kitu, huwa wanaanza na kasi kubwa, lakini haichukui muda wanaacha kufanya.
Kinachotokea ni watu hao wanakuwa hawajui ni jinsi gani ilivyo rahisi kuacha kufanya pale mtu anapokutana na changamoto au vikwazo.
Hivyo chochote unachoanza kufanya, jua kabisa ni rahisi kuacha pale unapokutana na magumu, na hivyo kutokukubali uishie njiani kirahisi.

Nguvu ya kufanya na kuacha kufanya ipo ndani yako, itumie vizuri kwa mafanikio yako.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuchagua kufanya yaliyo bora, na kuchagua kutokufanya yaliyo hovyo.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha