Kanuni ya mafanikio tunayoiishi kwenye KISIMA CHA MAARIFA ni MAARIFA SAHIHI + KUCHUKUA HATUA KUBWA = MAFANIKIO MAKUBWA.
Hakuna mafanikio makubwa kama hakuna hatua kubwa ambazo zinachukuliwa. Na kuchukua hatua kubwa bila ya kuwa na maarifa sahihi, ni kujiweka kwenye hali ya hatari sana.
Zipo faida nyingine nzuri sana za kuchukua hatua kubwa, ambazo unaweza kuzipata pale unapochukua hatua kubwa na zikawa msaada sana kwako.
Hatua kubwa zinakuondoa mafichoni na kukupeleka kwenye umaarufu na kujulikana. Watu wengi hufikiri umaarufu unatokana na kusema au kuonekana. Ni kweli vitu hivyo vinaweza kuleta umaarufu, lakini hautadumu. Watu wanaojulikana kweli, ni wale ambao wanachukua hatua kubwa kwenye kila wanachofanya. Wale wanaofanya kwa namna ya ziada, kuliko ilivyozoeleka, ndiyo wanaotafutwa na kila mwenye uhitaji. Chukua hatua kubwa na watu watakutafuta popote ulipo.
Hatua kubwa unazochukua zinaongeza sana thamani yako sokoni. Kadiri unavyochukua hatua kubwa, ndivyo unavyotoa matokeo makubwa na ndivyo thamani yako inakuwa kubwa zaidi. Kadiri thamani yako inavyopanda, ndivyo kiwango chako cha kulipwa kinapanda zaidi. Hivyo kwa wale ambao hawaridhiki na kipato wanachoingiza sasa, jawabu ni moja, chukua hatua kubwa, na siyo kupiga kelele au kulalamika.
Mwisho kabisa, hatua kubwa unazochukua, zinawafanya watu wajenge imani juu yako. Kadiri unavyochukua hatua, ndivyo watu wanavyoamini utachukua hatua zaidi. Hivyo inafika mahali watu hawahitaji kushawishiwa waamini utachukua hatua kubwa, wakiangalia matokeo yako tu wanajua wewe ni mtu wa kuchukua hatua kubwa.
Mara zote chukua hatua kubwa, na mafanikio kwako yatakuwa ni swala la muda na kiasi, na siyo swala la utapata au utakosa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,