Siku mpya,
Siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUFANYA NA KUJARIBU KUFANYA…
Kauli tunazotumia kwenye maisha yetu ya kila siku, zinaathiri sana mafanikio yetu.
Unaweza kupima kiwango cha mafanikio ya mtu kwa kauli ambazo anatumia, pale anapoahidi au kufanya maamuzi.
Mfano mzuri wa kauli ni kwenye kufanya.
Mtu anaposema NITAFANYA ni tofauti kabisa na kusema NITAJARIBU KUFANYA.
Ni kauli ambazo unaweza kuona zinalingana, lakini zina tofauti kubwa mno, ambayo inatenganisha wanaofanikiwa sana na wanaoshindwa.
Mtu anaposema NITAFANYA, anakuwa amejitoa kweli kufanya, anakuwa amejiweka kwenye nafasi ya kudaiwa pale ambapo hatafanya hivyo. Maana amesema atafanya, anaweza kubanwa kwa kauli hiyo na akafanua kweli.
Hivyo ije mvua lije jua, itabidi afanye, maana ameahidi kufanya.
Na ni ahadi ya aina hii ndiyo inawawezesha wengi kufanikiwa.
Lakini mtu anaposema NITAJARIBU KUFANYA, unajua kabisa mtu huyo hajajitoa kweli kufanya. Na hutakuwa na namna yoyote ya kumbana kufanua, kwa sababu alikuambia atajaribu kufanya, hivyo ukimghasi sana atakuambia alijaribu akashindwa.
Maana majaribio yana kushindwa na kufanikiwa, na hakuna anayefungwa kwa majaribio.
Tumia kauli ambazo zinakuweka kwenye nafasi ya kubanwa, kauli ambazo watu wanaweza hata kukushitaki kama hutatekeleza, na utaona jinsi ambavyo utajisikuma kufanya hata kama kuna uvivu unaokunyemelea.
Tumia kauli za kishujaa, kauli za mafanikio, kauli za kujiweka kwenye wakati mgumu, kauli ambazo usipotekeleza kuna vitu utapoteza.
Na kwa namna hiyo, utafanya, kwa viwango vya juu kabisa.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujitoa KUFANYA na siyo KUJARIBU KUFANYA.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha