Kama hujui fedha ya kula kesho inatoka wapi, hutapata usingizi usiku kucha, utakuwa na mawazo sana kuhusu kesho yako na maisha yataendaje.
 
Kama hujui mwezi utaishaje, yaani kipato kimeshaisha kabla ya malipo mengine kufika, hutapata usingizi mzuri usiku, mara zote utakuwa na mawazo maisha yako yataendaje mpaka kipato kingine kinapofika.
 
Kama huna uhakika wa maisha iwapo kazi au biashara uliyonayo sasa imetoweka ghafla, kila wakati utakuwa na wasiwasi na hofu. Inapotokea changamoto yoyote kwenye kazi au biashara yako, utapata mawazo sana yatakayokunyima usingizi kabisa.
 
Kuna kiwango cha fedha ambacho unapaswa kuwa nacho ili uweze kuwa na usingizi mzuri usiku. Kiwango cha fedha ambacho unajua chochote kinachotokea haiwezi kuwa na madhara makubwa kwako.
 
Kiwango hiki kinatofautiana baina ya watu kulingana na aina ya maisha ambayo kila mmoja wetu anayaishi. Hivyo jua kiwango chako ni kipi. Kwa wengi, kiwango hiki ni kiasi cha kuweza kuendesha maisha kwa miezi sita ijayo hata kama hakutakuwa na kipato kabisa. Wengine ni mwaka mmoja, wengine ni uhakika wa maisha kuendelea vizuri hata kama hawataweza kufanya kazi tena.
 
Jua kiwango chako na weka juhudi katika kukifikia, kwa sababu ukishafikia kiwango hiki, akili yako itatulia na utaweza kushughulika na mambo muhimu zaidi kwenye maisha yako.
 
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
 
Rafiki na Kocha wako,
 
Dr. Makirita Amani,