Ni vitu viwili ambavyo siyo tu vinakupotezea muda na nguvu kwenye kuvifanya, bali pia ni vitu vya kijinga sana kufanya, ambavyo havina mchango wowote kwenye mafanikio yako.

Hutaweza kufanikiwa kwa kushinda ubishani au ugomvi wako na wengine. Ubishani na ugomvi ni vitu ambavyo ukishaingia tu tayari umeshashindwa. Kwa sababu hata kama utashinda, bado utawapoteza wale ambao umewashinda, kwa sababu wengi huwa hawapokei vizuri kushindwa kwenye ubishi au ugomvi.

Hivyo epuka kabisa mabishano na ugomvi wa aina yoyote ile. Ni bora ukubaliane na watu kwa namna wanavyofikiri wao, uokoe muda na nguvu zako kwa matumizi mengine. Kuliko kukomaa na ubishi au ugomvi, halafu mwishowe unawapoteza kabisa wale unaobishana nao.

Kama kuna kitu unajua ni sahihi, lakini wengine wanajua kwa tofauti, ambapo siyo sahihi, unaweza kuchukua muda wako kuwaelewesha kile ambacho ni sahihi, ila ukiona hawaelewi, wanaleta ubishi, waache waendelee kuamini wanachotaka kuamini na wewe endelea na kile unachoamini.

Kama mtu anatafuta tu sababu ya kugombana na wewe, kaa naye mbali haraka sana, hata kama hilo litakufanya uonekane ni mwoga au dhaifu. Kwa kila ugomvi unaouepuka, unazidi kuwa imara wakati kwa kila ugomvi unaoshiriki unazidi kuwa dhaifu.

Na mwisho kabisa, sambaza upendo, upendo ndiyo jawabu la ugomvi mwingi. Kama utawapenda watu kwa namna walivyo, hutaweza hata kugombana nao. Wapende sana watu, na hilo litakuepusha na mambo mengi ya kupoteza muda wako kwenye mabishano na ugomvi usio na umuhimu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha