Rafiki yangu mpendwa,

Hakuna mtu anayejua umuhimu wa fedha kwenye maisha yako kuliko unavyojua wewe mwenyewe. Huenda ndiyo kitu kinachokuweka macho usiku kucha ukifikiria. Huenda ndiyo kitu unachofikiria muda mwingi wa maisha yako.

Hakuna ubaya wowote kwenye kutaka fedha zaidi, kwa sababu kuendesha maisha yetu kunahitaji fedha. Tatizo la fedha linakuja pale ambapo mtu unakuwa huna, na hapo ndipo changamoto nyingi zinapokushinda kutatua. Pia tatizo la fedha linakuwa kubwa sana pale unapokuwa unatumia njia ambayo siyo sahihi kutaka kupata fedha.

Kwa chochote ambacho unafanya kwenye maisha yako, kuna misukumo au hamasa za aina mbili.

Aina ya kwanza ni msukumo au hamasa inayotoka ndani yako. Hapa ni pale unapofanya kitu kwa sababu umechagua kufanya, kwa sababu unajua ni kitu muhimu kwako kufanya na kwa sababu unajua kuna thamani unaongeza kwenye maisha ya wengine.

Aina ya pili ni msukumo au hamasa inayotoka nje. Hapa ni pale unapofanya kitu ili kuonekana unafanya, au kwa sababu wengine wanafanya, au kwa sababu watu wanakutegemea ufanye hivyo. Pia unaweza kuwa unafanya ili upate kitu fulani unachotaka.

652d5-tangazo2bmasikini

Katika misukumo hii ya aina mbili, msukumo wa ndani yako ndiyo wenye nguvu sana, kwa sababu utafanya licha ya kinachoendelea nje yako. Lakini msukumo wa nje hauna nguvu kubwa, kwa sababu mazingira ya nje yakibadilika, basi na msukumo unabadilika.

Sasa kama unataka kupata fedha zaidi, tafiti zinaonesha kwa kutumia msukumo wa ndani unaweza kutengeneza fedha mara tatu zaidi ya unavyotumia msukumo wa nje.

Pale unapofanya kitu kwa sababu umechagua kufanya, kwa sababu unataka kuwasaidia wenye uhitaji au unataka kutoa mchango wako, utatengeneza kipato kikubwa kuliko pale unapofanya ili tu upate fedha ya kulipa gharama za maisha yako.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Power Of Motivation (Jinsi Unavyoweza Kufanikiwa Katika Mazingira Yoyote Yale)

Kama umeelewa vizuri hapo juu, unapofanya kitu kwa sababu tu unataka fedha, unapata fedha kidogo, kuliko kama utafanya kitu hicho hicho kwa msukumo kutoka ndani yako.

Na pale unapofanya kitu kwa msukumo wa ndani, haimaanishi kwamba hujali fedha, unajali sana, ila msukumo wa wewe kufanya ni mkubwa kuliko fedha, hivyo unakuwa umejiweka juu ya fedha, kitu ambacho kinakuwezesha kupata fedha kama unavyotaka.

Lakini unapofanya kwa ajili ya fedha pekee, utapata fedha, lakini utakuwa umeweka fedha juu yako, hivyo unakuwa umejiwekea ukomo wewe mwenyewe, ukishafika kiwango fulani cha fedha utaacha kufanya kwa sababu hamasa yako ilikuwa fedha pekee.

Rafiki, ujumbe wangu kwako ni huu, kuwa na msukumo wa ndani kwenye kila unachofanya, penda fedha na ihitaji, lakini isiwe msukumo pekee wa wewe kufanya kitu. Fanya unachofanya kwa msukumo wa ndani na utaweza kupata fedha kadiri utakavyo, na hutakuwa na ukomo wowote kwenye kipato unachoweza kutengeneza.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL