AMKA mwanamafanikio,
AMKA kwenye siku hii mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni siku nyingine ambayo tumepata nafasi ya kipekee kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari MAISHA KAMA MCHEZO…
Kama maisha ni mchezo, basi kuna vitu viwili muhimu sana unavyopaswa kuzingatia ili kushinda mchezo huu.

Kitu cha kwanza ni zijue sheria za mchezo, kila mchezo una sheria zake, na usipozijua kila wakati utazivunja na utapata adhabu ambazo zitakuzuia kushinda.
Maisha kama mchezo una sheria zake, ambazo ni muhimu sana kuzizingatia mara zote.
Zipo sheria za asili ambazo ukizifuata maisha yako yatakuwa bora, lakini ukizivunja, utaishi maisha yako yote kwa mahangaiko, usiweze kupiga hatua yoyote.

Kitu cha pili ni cheza mchezo wako,
Njia rahisi ya kishindwa kwenye mchezo wowote ule ni kucheza mchezo wa wengine.
Unashindwa kwa sababu wengine wanakuwa wanaujua vizuri mchezo wao kuliko wewe.
Hivyo ili kushinda mchezo huu wa maisha, cheza mchezo wako mwenyewe.
Ishi maisha yako na siyo maisha ya wengine,
Fanya yale yenye umuhimu na maana kwako na siyo yale wanayofanya wengine.
Kwa sababu ukikimbilia kufanya yale ambayo kila mtu anafanya, hata ukiyapata utajisikia bado hujakamilika, na itabidi uendelee kukimbiza mengine zaidi wakati ndani yako bado kumekosekana kilicho muhimu.
Unapofanya yale ambayo ni muhimu kwako unaridhika na yale matokeo unayopata, kwa sababu yanaendana na kile unachotaka.

Faida nyingine ya kucheza mchezo wako ni kwamba unaweza kujipendelea wewe mwenyewe, kitu ambacho ni kigumu kufanya unapocheza michezo ya wengine.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kujua sheria za mchezo wa maisha na kuchagua kucheza mchezo wako mwenyewe. Muda wako ni mfupi na ya kufanya ni mengi. Chagua yale muhimu zaidi kwako kufanya ili kuwa na maisha ya mafanikio.

#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha