Changamoto nyingi zinazotokana na kuajiri kwenye biashara, zinatokana na watu wanaotafuta kazi ya kufanya. Watu ambao wanakuambia wanaweza kufanya kazi yoyote na wanaoangalia ni nini wanalipwa pekee.

Hawa ni watu ambao unaweza kuwapata kirahisi sana, unaweza kuwalipa rahisi pia, lakini pia utawapoteza kirahisi na kazi yoyote wanayoiweka inakuwa ya urahisi, isiyo na thamani kubwa.

Watu bora kabisa wa kuwaajiri siyo wale wanaotaka kazi, bali wale wanaotaka kumiliki kitu, wale wanaotaka kutoa mchango wao, na wanajua kupitia kile unachowaajiri wafanye, wataweza kutoa mchango mkubwa kwa wengine.

Unahitaji kuwaajiri watu ambao wana njaa ya kuyamiliki maisha yao, wanaotaka kumiliki majukumu yao na kutaka kutoa mchango bora zaidi kwa wengine.

Hawa ni watu ambao hutahitaji kuwasimamia kwa karibu au kuwasukuma mara zote. Huhitaji kuwakumbusha majukumu yao kila wakati, kwa sababu wana njaa ya kukamilisha majukumu yao, wanakuwa wameshayakamilisha kabla hata hujawauliza.

Kupata aina hii ya watu ili uwaajiri, siyo rahisi, ila inawezekana sana. kama utakuwa na utulivu na kuwa tayari kufanya kazi na watu wengi, utakutana na wale wenye  sifa hizo, na ukishawapata, nenda nao vizuri kuhakikisha wote mnanufaika.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha