Wapo watu ambao wamekuwa wanahangaika kutafuta watu wa kuwatabiria au kuwanenea unabii kuhusu maisha yao. Lakini watu hao hawapaswi kwenda mbali ili kumpata nabii anayeweza kuwatabiria kwa usahihi wa asilimia 100.

Maisha ambayo unayaishi sasa, ni unabii ambao umetimia. Maisha uliyonayo sasa, hayajatokea kama ajali, badala yake yametengenezwa, kidogo kidogo, hatua kwa hatua.

Hukuamka siku moja na ukajikita kwenye madeni ambayo huwezi kuyalipa, badala yake ulianza kidogo kidogo kuwa na matumizi makubwa kuliko kipato chako, halafu ukakopa, halafu ukazidi kuongeza matumizi, ukazidi kukopa tena.

Hukuamka siku moja na ukakuta mahusiano yako ya kindoa ni mabovu na ndoa haiwezi kuendelea tena. Ulitengeneza kidogo kidogo mahusiano hayo mpaka yakafika hapo. Kuna vitu uliviona havipo sawa kwenye mahusiano hayo lakini ukakaa kimya, kuna mambo uliyapuuza kuhusu mwenza wako, kuna majukumu umeyakwepa na sasa umefika hapo ulipo sasa.

Najua ni rahisi kwako kunyoosha vidole, kwamba kama wazazi wako wangefanya hili au lile, kama serikali ingekuwa ya aina fulani, kama watu wangekuelewa, kama bosi wako angekujali, kama mwenza wako angekuwa mwelewa basi mambo yako yangekwenda kama unavyotaka.

Lakini siogopi kukuambia kwamba unajidanganya, hakuna yeyote mwenye mchango mkubwa wa hapo ulipofika sasa kukuzidi wewe. Mlaumu yeyote unayetaka, lakini mwisho wa siku jua kwamba wewe ndiye mtabiri mkuu wa maisha yako, utabiri wako kuhusu maisha yako umekuwa ukweli ambao unauishi sasa.

Ni kawaida yetu sisi binadamu kupenda kuangalia matokeo ya haraka, kwamba kinachotokea leo ni matokeo ya jana au tulivyofanya leo, na kama tunataka mambo mazuri basi tutayapata mara moja baada ya kuchukua hatua. Huku ni kujidanganya.

Maisha yako ni utabiri uliotimia, kwa sababu kila kinachotokea kwenye maisha yako sasa, ulishakiona kwenye mawazo yako, ulishakiweka kwenye mawazo yako. Wakati mwingine ulikiweka siyo kwa kukitaka,  bali kwa kukikataa.

Nikupe mfano, umewahi kusema sitaki kukutana na kitu fulani, halafu ndiyo ukakutana nacho? Au kujiambia hupendi vitu fulani na ukapata hivyo mara zote. Akili zetu huwa zinatuletea yale ambayo tunayafikiria kwa muda mrefu, iwe tunayafikiria kwa kuyataka au kwa kutokuyataka.

Ndiyo maana nakuambia maisha unayoishi sasa ni utabiri uliotimia, kwa sababu kuna namna ulishafikiria kila kinachotokea sasa.

Mfano mzuri ni kwenye kushindwa, hakuna mtu anayeshindwa kwa mshangazo, kila anayeshindwa anakuwa anajua kwamba atashindwa, anachofanya ni kukamilisha tu kwa vitendo ili asijisikie vibaya kwamba hakujaribu.

ANZA LEO KUTENGENEZA UTABIRI BORA.

Kwa namna nilivyokueleza kwamba maisha yako ni utabiri uliotimia, ni rahisi kuona kwamba huna namna bali kupokea kila kinachotokea kwenye maisha yako kama kinavyotokea.

Na hili halitakuwa sahihi, bali unachopaswa kufurahia ni kwamba, unayo nafasi ya kujitabiria vizuri zaidi ili kuwa na maisha bora. Unayo nafasi ya kutengeneza utabiri bora, wa yale mazuri yote unayotaka na kuyaruhusu yatawale fikra zako.

Anza kwa kutengeneza taswira ya aina ya maisha unayotaka, kisha weka taswira hiyo kwenye mawazo yako kila siku. Orodhesha yale yote ambayo ni muhimu kwako kila siku ili upate nafasi ya kuyafikiria zaidi. Kila unapokutana na kitu cha kukukatisha tamaa, kila unapokutana na ugumu, usiruhusu akili yako itawaliwa na fikra hasi na za kukosa, badala yake pata taswira ya maisha unayotaka, orodhesha kila unachotaka kwenye maisha yako.

Kwa namna ambavyo akili yako itaandamwa na mawazo ya maisha unayoyataka, haitakuwa na nafasi ya kuhangaika na vitu vingine. Na hapo itafanya kazi ya kuhakikisha utabiri unaojitengenezea unatokea kwenye maisha yako.

Nimalize kwa kukuambia rafiki yangu, haijalishi sasa upo wapi, unaweza kufika mbali zaidi kama utaanza kuchukua hatua sahihi leo, kwa kujitengenezea utabiri mpya na kuuishi kila siku ya maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha