“The wise person is safe and sound, and he cannot be affected either by any injury or by any insult.” – Seneca.
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
đź’ĄTAHAJUDI YA ASUBUHI.
“Mtu mwenye hekima yupo vizuri na salama. Hasumbuliwi na majeraha wala matusi.” – Seneca.
Kitu kikubwa kinachowatesa watu wengi kwenye maisha yao ni majeraha mbalimbali wanayoyapata kwa wengine, na hata matusi ambayo wanayapokea.
Lakini kama Wastoa wanavyosema, hakuna kitu cha nje chenye madhara kwa yeyote, bali jinsi ambavyo mtu anachukulia kinavyotokea.
Hivyo mtu yeyote anayekuumiza au kukutukana, kinachokuumiza wewe siyo alichofanya mtu huyo, bali jinsi wewe ulivyochukulia alichofanya.
Chukua mfano unapita njiani, ukakutana na mtu mwenye ugonjwa wa akili na akakutukana matusi makubwa, je hilo litakusumbua?
Kwa hakika hutasumbuka, maana unajua anafanya hivyo kwa kuwa ni mgonjwa.
Sasa kwa nini usichukulie hivyo kwa yeyote anayekutukana?
Kwa sababu matusi siyo kitu kizuri, hivyo yeyote anayekutukana, kwa hakika anaumwa, sasa kwa nini ikuumize wewe?
đź’ĄTAFAKARI YA MCHANA.
Mchana wa leo, pata muda wa kutafakari mambo ambayo wengine walishakufanyia wewe kwa lengo la kukuumiza au kukutukana.
Fikiria jinsi ulivyoyachukulia mambo hayo na ona kama ilikuwa na msaada kwako.
Kwa mfano kama mtu alikuumiza na wewe ukamwekea kinyongo, je hilo limekusaidia au kukuumiza zaidi?
Kama mtu amekutukana na wewe ukamrudishia matusi, je hilo limekutofautishaje na yeye?
Kinga pekee ya maumivu na matusi ni hekima,
Kama anavyotuambia Seneca, hakuna awezaye kumuumiza au iumdhalilisha mtu mwenye hekima.
Kwa sababu maumivu yanatokana na mtu kupoteza kitu fulani, mtu mwenye hekima hana cha kupoteza.
Kadhalika matusi yana lengo la kudhalilisha mtu, lakini mtu mwenye hekima hana cha kudhalilika nacho.
Kuwa mtu mwenye hekima, na hutasumbuka na vitu vidogo vidogo kama maumivu na matusi.
TAHAJUDI YA JIONI.
“The fact is that although all men are different from one another, the wise person regards them all as equal, on account of their equal stupidity. For if he lets himself just once descend to being disturbed by either injury or insult, he will never be able to be free from anxiety. And freedom from anxiety is the wise person’s hallmark.” – Seneca.
Japokuwa watu wanatofautiana, mtu mwenye hekima anajua watu wote wanafanana kwenye upumbavu. Hivyo mtu mwenye hekima haruhusu maumivu wala matusi kumsumbua, kwa sababu anajua kusumbuliwa na vitu kama hivyo ni kujinyima uhuru.
Jioni ya leo tahajudi kuhusu siku yako nzima,
Angalia tangu unaianza siku yako mpaka unaimaliza.
Je kuna mtu alijaribu kukuumiza kwa namna yoyote ile?
Je kuna mtu amekutukana au kukujibu vibaya kwenye siku yako ya leo?
Je umechukuliaje manbo hayo?
Kama umeruhusu yakuumize, unayo kazi ya kufanya kuhakikisha unakuwa na hekima zaidi.
Lakini kama hujayaruhusu yakuumize, upo kwenye njia nzuri ya kuwa na hekima.
Ukawe na siku bora aana ya leo, siku ya kuishi kwa hekima na kutokuruhusu chochote kikuumize, kwa sababu wenye hekima hawana cha kuwaumiza.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha