Rafiki yangu mpendwa,

Kama upo ujuzi mmoja ambao kila mtu anapaswa kuwa nao ili kufanikiwa kwenye maisha, basi ni kuuza. Wale wanaofanikiwa kwenye maisha yao ni wale ambao wanaweza kuuza vizuri kuliko wengine. Na siyo lazima kuwa kuuza kwenye biashara, bali kuuza ujuzi na uzoefu, kuuza maneno, kuuza mipango na mengine mengi. Ili kuweza kumshawishi mtu yeyote akubaliane na wewe, lazima uwe muuzaji mzuri.

Kwenye biashara, eneo muhimu sana ni mauzo. Mauzo ndiyo yanayoleta fedha kwenye biashara na fedha hizo ndizo zinazoiwezesha biashara kwenda vizuri. Hivyo eneo muhimu la kukazania kwenye biashara ni eneo la mauzo.

Watu wanatofautiana kwenye kuuza. Kuna watu ambao ukiwapa chochote wanaweza kukiuza kwa yeyote, na wapo wengine ambao hawawezi hata kumshawishi mtu kununua. Wengi ambao wanajiona hawapo vizuri kwenye mauzo, wamekuwa wanajiambia hawawezi kufanikiwa kwenye biashara.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Lakini huo siyo ukweli, kila mtu anaweza kufanikiwa kwenye biashara anayoifanya, hata kama siyo mzuri kwenye mauzo, yaani kwa nje haonekani sana kama muuzaji.

Kuna kitu kimoja ambacho mtu akiwa nacho anaweza kuuza zaidi hata kama siyo muuzaji mzuri. Kitu hicho ndiyo tunakwenda kujifunza leo na kuweza kukitumia ili tuweze kuuza vizuri chochote tunachouza kwenye maisha yetu.

Kitu kimoja kitakachokuwezesha kuuza zaidi ni kuamini kwenye kile tunachouza. Imani yako kwenye kile unachouza itakuwezesha kuuza zaidi hata kama wewe siyo muuzaji mzuri.

Watu wengi huwa wanafikiri kinachowafanya wateja wanunue ni maneno, na ndiyo maana huwa wanaongea sana mpaka hata kudanganya ili tu watu wanunue. Lakini ukweli ni kwamba, kinachowafanya wateja wanunue ni imani wanayoweza kuijenga juu yako. Na wateja wanajenga imani juu yako kulingana na jinsi ambavyo wewe unaamini kile unachouza.

Kila mtu anaweza kudanganya kwa maneno, lakini imani ipo wazi, huwezi kudanganya. Kwa jinsi unavyoelezea kitu, mtu ni rahisi kuona kama ni kweli unaamini kitu hicho au unasema tu.

Wateja wanapojua kwamba unaamini kwenye kile unachouza, wanakuamini na wao wanajiamini zaidi kufanya maamuzi. Wanashawishika kununua kwa sababu wanajua wamepata kitu sahihi.

Kama huamini kwenye kile unachouza, kama una wasiwasi wowote juu ya unachoahidi wale unaowauza, wasiwasi huo utaonekana wazi kwa wateja wako na hawatakuamini au kujiamini wao wenyewe na kununua.

Ni wajibu wako kuamini kwenye kile unachouza, kuwa na imani isiyoyumbishwa juu ya kitu hicho, kuwa na uhakika kwamba kitu hicho kinafanya kile unachosema kinafanya. Imani yako inapaswa kwenda mbali zaidi kwa kuamini kwamba mteja anafanya makosa makubwa sana kama hatanunua kile unachouza.

SOMA; Usisingizie Fedha Tena; Njia Saba Za Kupata Mtaji Wa Kuanza Biashara Hata Kama Huna Pa Kuanzia Kabisa.

Swali ni je unawezaje kujenga imani yako na ya wateja wako kwenye kile unachouza?

Majibu ni rahisi;

Moja; penda kile unachofanya, usifanye kwa sababu ya fedha pekee, fanya kwa sababu unapenda kufanya, fanya kwa sababu unajali, fanya kwa sababu kuna mchango unaotoa kwa wengine.

Mbili; kuwa mtumiaji wa kwanza wa kile unachouza, hakikisha wewe mwenyewe unaweza kutumia, au unaweza kumshauri mtu wako wa karibu kabisa, unayempenda sana atumie. Kwa maneno mengine usiuze kitu ambacho wewe mwenyewe huwezi kutumia au huwezi kumpa mtu wako wa karibu atumie.

Tatu; toa uhakika wa unachouza na mpe mteja nafasi ya kurudisha iwapo alichonunua hakitamfaa au hakitafanya kazi kama alivyotegemea. Mfanye mteja aone hana cha kupoteza anaponunua kwako.

Nne; jua tatizo la mteja unalotatua na elezea kile unachouza kwa namna kinavyotatua tatizo hilo. Usieleze sifa za kitu pekee, bali eleza namna zinatatua tatizo la mteja wako.

Tano; usiwaseme vibaya washindani wako, usihangaike kuwashinda wengine, kama unachouza ni kizuri kweli, huna haja ya kuhangaika na wengine wanauza au kusema nini. Lakini kama huamini kwenye unachouza, itabidi uanze kuwakosoa na kuwasema vibaya wengine, ili kumfanya mteja wako aone wewe upo sahihi, lakini hata unapowasema vibaya wengine, mteja anajua kuna shida kwenye biashara yako.

Rafiki, amini kwenye kile unachouza na utaweza kuuza zaidi hata kama unajiambia wewe siyo muuzaji mzuri. Anza na hayo matano niliyokushirikisha na utaweza kujenga imani nzuri kwako na kwa wateja wa kile unachouza.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL