Ukiwa unatembea kwenye njia ya kawaida, huna hofu kwamba utadondoka na kuumia, kwa sababu umbali kati yako ana ardhi siyo mkubwa, hivyo hilo halikupi mawazo sana, unakazana na kutembea na mawazo yako yanakuwa kwenye mambo mengine muhimu, na siyo kufikiria kuhusu kuanguka.

Lakini ukiwa unatembea kwenye ukuta mwembamba, ambao upo kwenye eneo lenye urefu mkubwa kutoka ardhini, ambapo ukianguka utaumia sana, akili yako yote inakuwa inafikiria kwa jinsi gani usianguke na unajitengenezea hofu kubwa sana kuhusu kuanguka. Utatumia muda mwingi kuangalia kule chini ambapo unaweza kudondokea, na hilo litakupa hofu zaidi.

Sasa ukiangalia mifano hiyo miwili, yote inahusisha kutembea, kitu ambacho unakifanya kila siku, lakini mmoja umeongeza mazingira hatarishi, lakini hayabadili kutembea kwako. Kinachobadili kutembea kwako ni hofu unayojijengea na kinachojenga hofu ni wewe kuangalia zaidi ile hatari kuliko kuangalia kutembea kwako vizuri.

Kwenye maisha, hivi ndivyo wengi wanavyotengeneza hofu zao na kupelekea kushindwa. Wanaangalia zaidi hatari zinazowakabili, badala ya kuangalia kile wanachopasa kufanya ili kupata kile wanachotaka. Wengi wanakazana kuangalia hatari zinazowakabili, kuangalia jinsi wanavyoweza kushindwa na jinsi watakavyoumia, na hilo linawapa hofu kubwa, inayowapelekea wengi washindwe kabla hata hawajaanza.

Njia pekee ya kuepukana na hofu za aina hii, ni kuacha kuangalia zile hatari na kupeleka akili, mawazo, imani na nguvu zako zote kwenye kile unachopanga kufanya.

Unapaswa kuweka umakini wako kwenye kile ulichopanga kufanya kiasi kwamba hupati kabisa nafasi ya kufikiria visivyo muhimu au kuangalia changamoto mbalimbali unazoweza kukutana nazo.

Hili halimaanishi kwamba unajifanya kama huoni hatari zilizopo, au unajifanya kama huwezi kushindwa, hayo yote unajua yanaweza kutokea, lakini huyapi nafasi kwenye fikra, imani na hata muda wako. Wewe unapeleka umakini wako wote kwenye kile unachopaswa kufanya, na kama utakifanya vizuri, basi utavuka hatari nyingi unazohofia.

Kujitengenezea hofu kwa kufikiria yale mabaya yanayoweza kutokea ni kujiweka kwenye nafasi ya kushindwa au hata kutokuanza kabisa. Lakini kupeleka umakini wako wote kwenye kile unachoweza kufanya, unaondokana na hofu na kama ukifanya vizuri, utavuka kila aina ya hatari uliyokuwa unaiona.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha