Kuna vifaa viwili muhimu sana unapaswa kuwa navyo kila wakati wa maisha yako, yaani kila muda, unapaswa kuwa na vifaa hivi. Utembee navyo popote ulipo, unapolala viwe pembeni yako.
Najua unafikiria kifaa kimoja ambacho ni kama umeshafunga nacho ndoa kwa sasa, maana huenda unakipenda kuliko vitu vingine, kifaa hicho ni simu. Yaani nasema unachofikiria kimoja ni simu yako, ambayo huenda ndiyo kitu cha kwanza unachoshika pale unapoamka na kitu cha mwisho kushika kabla hujalala. Kama watu wangekuwa wanapoteza nywele moja kila wanapogusa simu zao, basi tungekuwa na watu wengi sana wenye upara.
Sasa turudi kwenye vifaa viwili vya maajabu, ambavyo leo nakwenda kukushirikisha, ambavyo nakuambia vina nguvu ya kushinda hofu na kukata tamaa.
Vifaa hivi ni kijitabu na kalamu.
Umejisikiaje baada ya kujua vifaa hivi, ambavyo huenda hukutegemea sifa zote nilizokuwa namwaga ni kwa vifaa vya kawaida kiasi hicho, vifaa ambavyo huenda hujawahi kuvitumia kwa muda mrefu sana? Unajisikia kama nimekupotezea muda? Subiri nikufafanulie kwa kina umuhimu wa vifaa hivi na jinsi unavyoweza kuvitumia kupiga hatua kwenye maisha yako.
Kijitabu na kalamu ya kuandika ni vifaa viwili ambavyo unaweza kuvitumia kufanya makubwa sana kwenye maisha yako. Kwa sababu ni vifaa ambavyo vitakuwezesha wewe uitumie akili yako vizuri kwa kuiwezesha kufikiri makubwa, kutunza yale muhimu na kufikia makubwa pia.
Nikuulize swali, ni mara ngapi umewahi kupata wazo zuri kweli, wazo ambalo ulijiambia utalifanyia kazi mara moja, halafu baadaye unakuja kujikuta umesahau kabisa wazo hilo? Ni mara nyingi, hata kwangu huwa inatokea mara nyingi, licha ya kuwa na vifaa hivyo viwili.
Kwa kutumia kijitabu chako na kalamu, na ukaandika kila wazo unalopata, unatunza mawazo yako vizuri na pia unaipa akili yako uhuru wa kufikiri zaidi kwa sababu unapoandika mawazo yako ni kama unayapakua kutoka kwenye akili yako na kuiacha akili yako ikiwa huru.
Sasa tukirudi kwenye somo nililokuandalia leo, la kutumia kijitabu chako na kalamu kuishinda hofu na kukata tamaa. Unachofanya ni kuyaandika malengo na maono yako makubwa mara kwa mara kwenye siku yako. Kwanza unafanya hivyo pale unapoamka, kisha unafanya tena unapokaribia kulala. Na kwenye siku yako, kila unapokutana na hali ya kukukatisha tamaa, kila unapokutana na hali ya hofu, unachofanya ni kuchukua kijitabu na kalamu yako na kuyaandika upya malengo na maono yako makubwa.
Fanya hivyo hata kama ni mara kumi kwa siku, haijalishi, wewe andika. Sasa unapoandika, unailazimisha akili yako ifikirie kuhusu kile unachotaka na siyo kile unachohofia, na hapo moja kwa moja hofu yako inapotea yenyewe.
Hofu ni kama moto, ili moto mkubwa uwake, unaanza na moto mdogo, halafu moto huo unaendelea kujichochea zaidi mpaka unakuwa moto mkubwa. Sasa unapopata wazo moja la hofu au kukata tamaa, linakaribisha wazo jingine na jingine na jingine tena, ndani ya muda mfupi unajikuta umeshajiambia huwezi, haiwezekani na hakuna haja ya kujisumbua.
Lakini unapotumia kijitabu na kalamu yako kuandika maono yako makubwa pale hofu inapoanza, inakuwa ni kama umemwaga maji kwenye moto unaoanza, unazima haraka kabla haujajichochea na kuwa mkubwa zaidi.
Kabla sijakuacha uendelee na mengine, najua kuna kitu unafikiria kwenye akili yako, kwamba huhitaji kuwa na kijitabu na kalamu, kwa sababu unaweza kutumia simu yako kuandika chochote. Na hapo hapo nikuambie huwezi kulinganisha simu na kijitabu na kalamu. Haijalishi umenunua simu milioni na kijitabu na kalamu ni elfu moja, kitendo cha kuandika kwa kalamu kwenye kijitabu chako, siyo sawa kabisa na kuandika kwenye simu yako.
Hivyo hakikisha wakati wowote, unakuwa na kijitabu na kalamu karibu yako, hii ni hazina ambayo itakusaidia sana kwenye nyakati ngumu na nyakati nzuri pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,