“Ignore what other people are doing. Ignore what’s going on around you. There is no competition. There is no objective benchmark to hit. There is simply the best you can do — that’s all that matters.” -Ryan Holiday
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nyingine bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari FANYA KILICHO BORA, ACHA KUSHINDANA..
Watu wengi wamekuwa wanapotea na kutokufanikiwa kwa sababu wanakuwa wameachana na njia zao na kuanza kukimbizana na njia za wengine.
Kila unapoacha kuangalia kile unachoweza kufanya wewe na kuangalia wengine wanafanya nini, unajitoa kwenye njia ya ushindi.
Kila unapojilinganisha na wengine, kila unapokazana ili kuwashinda wengine, unajipoteza wewe mwenyewe.
Kwa sababu wewe pekee ndiye mwenye safari ya mafanikio uliyonayo wewe, hakuna mwingine mwenye safari hiyo.
Puuza yale ambayo wengine wanafanya, puuza nini kinaendelea kwa wengine na achana kabisa na kushindana.
Unachohitaji ni kufanya kile kilicho bora kabisa, kadiri ya uwezo uliopo ndani yako na kutoruhusu muda wako upotelee kwa yale yasiyo muhimu.
Mafanikio yako kwenye maisha siyo kuwashinda wengine, bali kufanya kile ambacho kipo ndani ya uwezo wako kufanya, na kwenda hatua ya ziada zaidi.
Kwa zama hizi, ambapo mitandao ya kijamii imekuwa sehemu ya kuonesha kila kinachoendelea kwenye maisha ya watu, ni rahisi sana kujilinganisha na wengine na kuona labda wewe bado sana.
Achana na hilo haraka na kazana kufanya kilicho bora zaidi, kadiri ya uwezo wako.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuchukua hatua kubwa sana kulingana na uwezo wako na malengo na mipango uliyojiwekea. Leo ikawe siku yako ya kupunguza kufuatilia maisha ya wengine na kuanza kuyafuatilia maisha yako kwa undani zaidi.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha