“Keep your fears to yourself, but share your courage with others.” ― Robert Louis Stevenson
Rafiki,
Ile siku ambayo uliipangilia kwa mambo mengi,
Mengine mapya na mengine umeahirisha,
Tayari imewadia.
Hivyo leo, nenda kafanye yale uliyojiahidi utafanya, na chochote unachoweza kufanya leo, usikisogeze kesho.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari FICHA HOFU, ONYESHA UJASIRI…
Kitu kimoja cha kushangaza kuhusu sisi binadamu ni hiki; tunapokuwa na hofu ya kitu fulani, huwa hatutulii nayo, tunakazana kuisambaza kwa kila mtu kwa kila namna.
Lakini tunapokuwa na ujasiri wa kitu, tunapokuwa na uhakika wa jambi fulani, huwa hatusambazi kama tunavyosambaza hofu, bali tunakaa nao wenyewe.
Sasa unachopaswa kufanya kwenye maisha yako ni kinyume na ulivyozoea.
Unapokuwa na hofu juu ya jambo lolote, kaa nayo mwenyewe, usikazane kuwasambazia wengine.
Hofu zako, ambazo kwa asilimia 90 ni za uongo na hazina msingi kabisa, hazina msaada wowote kwa wengine.
Lakini unapokuwa na ujasiri, unapokuwa na uhakika, huo sambaza kwa wengine, kwa sababu huu unawahamasisha watu na kuwawezesha kupiga hatua zaidi kwenye maisha yao.
Kadhalika, ukiona mtu anasambaza zaidi hofu kuliko ujasiri, kaa naye mbali, huyo ni mtu sumu, ambaye anasambaza hofu lakini ujasiri anabaki nao yeye mwenyewe.
Uzuri wa hili ni kwamba, unapoacha kusambaza hofu uliyonayo inakosa nguvu ndani yako na kupotea. Lakini ukiisambaza, inapata nguvu zaidi na kukua. Unaweza kuwa na hofu kidogo, ukasambaza kwa wengine na wao wakaiongeza ikawa kubwa kiasi cha kukutisha zaidi wewe kuliko ulivyokuwa umetishika mwanzo.
Rafiki, kuwa na siku bora sana ya leom siku ya kuficha hofu zako na kukaa nazo mwenyewe na kusambaza ujasiri na uhakika uliopo ndani yako.
#SambazaUjasiriSiyoHofu #SambazaUpendo #IshiLeo #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha