Siku za nyuma, chakula ambacho kilikuwa kinaogopeka sana kiafya kilikuwa ni mafuta. Tafiti za kipindi hicho zilionesha mafuta yanasababisha magonjwa ya moyo kama presha ya kupanda na pia magonjwa kama kisukari. Hivyo mafuta yaliogopewa sana.
Lakini kwa sasa, chakula kinachoogopeka zaidi ni sukari. Tafiti nyingi za sasa zinaonesha sukari inasababisha magonjwa mengi kwenye miili yetu na kuchochea mengine pia. Magonjwa ya moyo kama presha ya kupanda, kisukari na hata saratani, zinachochewa zaidi na sukari.
Pia sukari imekuwa kisababishi kikuu cha watu kuwa na uzito uliopitiliza.
Tunapenda sana sukari, hii ni kwa sababu ni tamu na inameng’enywa haraka na mwili kutupatia nguvu. Ugali na sukari ya kawaida vyote ni kundi moja la chakula, yaani wanga. Lakini ukila ugali itakuchukua muda mpaka wanga wake umeng’enywe na sukari ipatikane. Lakini ukila sukari ya kawaida, mara moja inameng’enywa na unaipata kwenye mwili.
Akili zetu pia zina sukari yake, kwa sababu tunajua chakula cha akili ni maarifa na taarifa, kuna sukari ya akili, ambayo ni rahisi kupata na kumeng’anya, lakini ina madhara makubwa kwenye akili zetu, kama ilivyo sukari kwenye miili yetu.
Sukari ya akili ninayoizungumzia hapa ni habari. Habari ni rahisi kusikia, rahisi kujadili, rahisi kukosoa, rahisi kulalamika na rahisi kuingiwa na hisia kulingana na habari husika. Lakini hazina msaada mkubwa kwako kuweza kupiga hatua kubwa. Lakini bado unataka kupata habari, akili yako ikishazoea habari, utahakikisha kila siku unaamka na habari na unamaliza siku yako na habari. Utatafuta magazeti yote na usome hata habari za mbele tu. Ukisikia habari mpasuko unahakikisha unaijua ni nini. Ukikosa habari kwa muda tu unaona kama dunia inakuacha.
Chakula sahihi cha akili zetu ni maarifa ambayo yanapatikana kwa kusoma vitabu na kujifunza vitu vyenye manufaa kwetu kulingana na kazi au biashara ambazo tunafanya. Wengi hawapendi chakula hichi, kwa sababu kama ilivyo ugali kwenye mwili, upatikanaji wa maarifa utakutaka umeng’enye yale maarifa unayoyapata ili uweze kuondoka na cha kufanyia kazi. Nguvu ambayo huihitaji kwenye habari, maana tayari imeshameng’enywa.
Habari haikutaki wewe ufikiri kwa kina na kuona kipi cha kufanya, maana habari tayari imekamilika, inashika tu hisia zako. Lakini maarifa halisi unayopata kwenye vitabu au kujifunza kwa njia nyingine, yanakutaka ufikiri kwa kina, yanakutaka uumize akili yako ili kuweza kujua hatua sahihi kwako kuchukua.
Ni urahisi huo wa habari, ambao umewafanya watu wengi kwa sasa kuwa wazembe, wasiweze kutumia akili zako kufikiri na kuja na matatizo ya changamoto wanazopitia.
Na uwepo wa mitandao ya kijamii ndiyo kabisa umeharibu akili za wengi, maana kwa sasa watu hawawezi tena kufanya kitu kwa kufikiri, badala yake wanaitumia mitandao ya kijamii kuangalia wengine wanafanya nini au kulalamikia kile wanachopitia.
Kama ambavyo sukari inavyochochea magonjwa mengi ya akili, habari na mitandao ya kijamii vinachochea uzembe wa akili na tafiti zinaonesha pia kwamba magonjwa ya akili kama msongo wa mawazo na sonona yamekuwa yanachochewa zaidi na mitandao ya kijamii.
Jikinge na sukari hii ya akili ambayo inakufanya uwe mzembe. Kazana na chakula sahihi cha akili ambacho ni maarifa, ambayo utayapata kwa kusoma vitabu, kujiunga na kozi mbalimbali au kuhudhuria semina ambazo zinakufundisha kitu kinachofikirisha akili yako na ukaweza kuchukua hatua fulani.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,