Tunapokuwa tunaanza kufanya kitu, huwa tunakuwa ni watu wa kujifunza. Tunakuwa tunajua hatujui na hivyo kuweka juhudi katika kujifunza ili kuweza kufanya vizuri zaidi.

Ni kiu hii ya kujifunza ndiyo inayotuwezesha kuwa bora zaidi, kuweza kufanya vizuri zaidi na kupata matokeo bora zaidi. Lakini kadiri tunavyokuwa bora, kadiri tunavyopata matokeo mazuri, hatari mpya inajitokeza kwetu.

Pale tunapoanza kujifikiria ndani yetu kwamba tumeshakuwa bora, pale tunapoona hatuna tena kipya cha kujifunza, pale tunapodhani kwamba tunaweza kufanya kwa ubora bila hata ya kuweka juhudi kubwa, hapo ndipo hatari kubwa sana ilipo.

Hatari kubwa unayokuwa unaitengeneza ni ya kuanguka, hatari ya kushindwa, kwa sababu unapofikiri kwamba umeshakuwa bora, unaacha kuwa bora ziadi na kuanguka.

Haimaanishi kwamba hupaswi kuwa bora, badala yake hupaswi kuufanya ubora uwe kikwazo kwako kuwa bora zaidi. Haijalishi umekuwa bora kiasi gani, haijalishi unafanya vizuri kiasi gani, bado unayo nafasi ya kufanya kwa ubora zaidi, bado unayo nafasi ya kuwa vizuri zaidi na zaidi.

Na utaweza kuendelea kuwa bora zaidi kama utakuwa tayari kujifunza zaidi, hata kama tayari unafikiri umeshakuwa bora sana.

Utaweza kufanya vizuri zaidi kama utakuwa tayari kuweka juhudi zaidi, hata kama umeshazoea namna ya kufanya. Unapojaribu njia mpya, unapoweka ubunifu na utofauti, hapo ndipo unapoweza kufanya zaidi.

Kila siku, fanya kile unachofanya kama ndiyo siku ya kwanza kwako kufanya, uwe na hamasa unayokuwa nayo siku ya kwanza, uweke juhudi unazoweka siku ya kwanza na uwe tayari kujifunza kama unavyokuwa kwenye siku ya kwanza.

Ukienda hivi kwa maisha yako yote, hutaanguka bali kufanikiwa zaidi, utakutana na magumu lakini utaweza kuyavuka, hakuna changamoto itakayokushinda na mafanikio yako yatakuwa ya kudumu.

Lakini kama utajisikiliza au kuwasikiliza wale wanaokuzunguka, wanapokuambia tayari wewe ni bora na huhitaji kujifunza tena au kuweka juhudi zaidi, utakuwa umetengeneza njia rahisi kwako kushindwa zaidi.

Kila siku mpya kwako, ni siku ya kwanza kwenye kufanya kile unachofanya, na siku ya kwanza ndiyo siku bora kwa mafanikio yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha