Kuna aina kuu mbili za mbio, kuna mbio fupi na mbio ndefu. Kwenye mbio fupi, mwenye kasi zaidi ndiye anayeshinda. Lakini kwenye mbio ndefu, anayekaa kwenye mbio muda mrefu zaidi ndiye anayeshinda. Ukiangalia mchezo wa mbio ndefu, huwa wanaanza watu wengi, lakini kadiri mbio zinavyokwenda, wengi wanaishia njiani. Mpaka kufika mwisho, wanakuwa wamebaki wachache sana.
Maisha ni kama mchezo wa mbio ndefu, na siyo mbio fupi. Kwenye maisha, anayefanikiwa ni yule anayekaa kwenye mbio kwa muda mrefu, na siyo yule mwenye kasi sana. Yule ambaye anapangilia mbio zake kwa namna ambayo anaendelea kuwa kwenye mbio miaka na miaka ndiye anayefanikiwa.
Vitu vingi kwenye maisha huwa vinaanzwa na wengi, lakini wengi huanza kwa mategemeo ya kufanikiwa haraka. Wanapokosa mafanikio hayo ya haraka wanakata tamaa na kuacha, kisha kwenda kuanza kitu kingine. Wanafanya hivyo kwa miaka mingi, mpaka wanakuja kujikuta umri umeenda na hakuna kikubwa walichofanya.
Lakini kama unataka mafanikio kwenye kitu chochote unachofanya kwenye maisha yako, ingia ukijua utafanya kwa muda mrefu. Ondokana kabisa na mawazo ya mafanikio ya haraka au ya muda mfupi. Ondokana na mawazo ya kuingia na kutoka mara moja.
Chochote unachochagua kufanya, jipe muda, fikiria kwa muda mrefu na jua ni swala la muda tu mpaka kufikia mafanikio yako, kama kweli utakuwa unafanya.
Unapoingia kwenye kazi, usifikirie mafanikio ya haraka, weka muda wako, weka kazi, weka juhudi kubwa na jua kadiri unavyokwenda, ndivyo nafasi ya kufanikiwa kwako inakuwa kubwa zaidi.
Unapoingia kwenye biashara, achana na mawazo ya mafanikio ya haraka, ingia ukifikiria kwa muda mrefu, ukijitoa kuweka juhudi kwa muda mrefu na kufanya biashara hiyo kwa muda, ni kwa njia hiyo ndiyo unafikia mafanikio makubwa.
Unapowekeza, fikiria kwa muda mrefu, usiangalie matokeo ya haraka, labda ni thamani ya uwekezaji inakua au kushuka, fikiria kwa muda mrefu na kadiri muda unavyokwenda, thamani ya uwekezaji wako itazidi kukua zaidi.
Kama ipo tiba moja ya uhakika ya mafanikio basi ni muda. Kama mtu utakuwa umejitoa kweli kufanikiwa, kama utakuwa tayari kuweka juhudi sana na kutokukata tamaa, basi kitu pekee kinachohusika na mafanikio yako ni muda. Kadiri unavyoweka muda kwenye kile unachofanya, ndivyo unavyoyatengeneza mafanikio yako.
Ukishajua ni nini hasa unataka kwenye maisha yako, na ukishajitoa kweli kulipa gharama unayopaswa kulipa ili kupata unachotaka, kinachobaki upande wako ni muda tu. Weka muda na utaweza kupata mafanikio makubwa sana kwenye chochote unachotaka. Hakuna kinachoweza kushindana na muda na ikashinda. Weka muda upande wako na utakuwa na uhakika wa ushindi kwenye chochote unachofanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,