Rafiki yangu mpendwa,

Karibu sana kwenye TANO ZA JUMA, makala ambayo nakukusanyia mambo matano muhimu sana kwako kujifunza na kuchukua hatua ili maisha yako yaweze kuwa bora.

Kama ambavyo nimekuwa nakusisitiza, kipimo bora cha muda kwako, kwa upande wa mafanikio ni juma, juma moja, lenye siku saba na masaa 168 ni kipimo kizuri sana kwako kujua kama unasonga mbele au unarudi nyuma.

Hivyo kila unapomaliza juma, kaa chini kutafakari juma lako, pia kabla hujaanza juma, lipangilie. Zoezi hili dogo litakuwa na manufaa makubwa sana kwako.

MASAA MAWILI YA ZIADA

Kwenye juma hili namba 42 tunalomaliza, nimekuandalia tano za juma zenye hatua muhimu sana kwako kuchukua ili kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa.

Karibu sana kwenye tano za juma namba 42 kwa mwaka huu 2018.

#1 KITABU NILICHOSOMA; NJIA 52 ZA KUWA NA MAISHA MAZURI

Lipo swali moja ambalo watu wamekuwa wakijiuliza tangu binadamu tumeanza kuishi kama jamii iliyostaarabika. Kwa zaidi ya miaka 2000 imepita, swali kubwa ambalo watu wamekuwa wanajiuliza ni jinsi gani mtu unaweza kuwa na maisha mazuri.

Jinsi gani mtu unaweza kuishi vizuri? Maisha mazuri yanajumuisha nini? Lipi jukumu la fedha kwenye maisha mazuri? Haya ni maswali ambayo watu wamekuwa wakijiuliza tangu enzi na enzi.

Falsafa mbalimbali na hata dini zimekuwa zinajaribu kujibu swali hili, lakini bado watu hawajapata jawabu la uhakika. Na moja ya sababu zinazopelekea jibu la uhakika lisipatikane ni mabadiliko makubwa yanayotokea kwenye mazingira yetu kila siku.

Kitu kilichofanya maisha yawe mazuri miaka 100 iliyopita, hakiwezi kuyafanya maisha yawe mazuri leo hii. Na miaka kumi ijayo, mambo yatakuwa tofauti sana na yalivyo sasa.

Pamoja na mazingira ya nje kubadilika kwa kasi, ndani yetu bado hatujabadilika sana, jinsi tunavyofikiri na kufanya maamuzi hatuna tofauti kubwa na watangulizi wetu walioishi miaka mingi iliyopita. Na ndiyo sababu licha ya maendeleo kuwa makubwa, watu bado wanafanya makosa yanayowagharimu sana.

Mwandishi Rolf Dobelli baada ya kuona changamoto hii ya maisha, ametushirikisha njia 52 ambazo amekuwa anazitumia yeye kufanya maamuzi sahihi na kuweza kuwa na maisha bora. Njia hizi amezitengeneza kutoka kwenye vyanzo vikuu vitatu; tafiti za kisaikolojia, falsafa ya ustoa na misingi ya uwekezaji wa wawekezaji wawili wenye mafanikio makubwa, Warren Buffet na Charlie Munger.

Karibu nikushirikishe njia hizi 52 za kukuwezesha kuwa na maisha mazuri, kwa kufanya maamuzi sahihi kulingana na hali unayokutana nayo.

Kwenye uchambuzi huu nitakushirikisha njia hizo 52 kwa ufafanuzi wa kina zaidi unaweza kusoma kwenye kitabu, au kama upo kwenye KISIMA CHA MAARIFA, unaweza kuuliza na nikakupa ufafanuzi wa ndani zaidi kwa baadhi ya njia ambazo huenda hujazielewa.

Na hizi ndizo njia 52 za kuwa na maisha mazuri, maisha yenye furaha wakati wote bila ya kujali unapitia nini.

 1. Ukipoteza fedha chukulia kama umetoa sadaka au umemsaidia asiyejiweza, hilo litakuzuia usiumizwe na kupotea kwa fedha.
 2. Hujakamilika na wala hakuna kilichokamilika, kila kitu kinahitaji kufanyiwa marekebisho na kuboreshwa zaidi.
 3. Jiweke msimamo kwenye maeneo muhimu ya maisha yako, ni vitu gani utafanya au hutafanya hata iweje, kisha ishi msimamo huo bila ya kuuvunja.
 4. Kwenye kila kosa unalofanya kwenye maisha yako, jiulize ni kwa jinsi gani ulifikia kwenye kosa hilo, ili wakati mwingine usirudie.
 5. Kuwa makini na teknolojia zinazoahidi kuokoa muda, nyingi zinaishia kukupotezea muda zaidi. Kama kitu hakina mchango mkubwa kwako na maisha yanaweza kwenda bila ya kitu hicho, achana nacho, kinakupotezea muda.
 6. Njia rahisi ya kuwa na maisha mazuri ni kuepuka kufanya makosa ya wazi. Kama unajua kitu siyo sahihi, usifanye.
 7. Sehemu kubwa ya mafanikio uliyonayo yametokana na bahati na siyo juhudi zako binafsi. Kama ungezaliwa miaka 100 iliyopita, usingeweza kuwa na maisha uliyonayo sasa.
 8. Usiziamini sana hisia zako, huwa zinakudanganya ili ufanye kile ambacho siyo sahihi. Lakini amini hisia za wengine, maana watu huendeshwa kwa hisia kuliko kufikiri.
 9. Ni muhimu kuwa wewe, lakini siyo lazima uweke wazi kila kitu kuhusu wewe kwa sababu unataka kuwa halisi. Jichukulie wewe kama nchi, ambayo ina mambo yanayokuwa wazi na yasiyokuwa wazi.
 10. Sema hapana mara nyingi uwezavyo na utalinda muda wako, pamoja na kuepuka mizigo isiyokuwa na maana kwako. Na pia hakuna kikubwa utakachokosa kwa kusema hapana mara nyingi uwezavyo.
 11. Unachoona kwa wengine na kukitamani, siyo bora kama unavyofikiria. Huenda maisha yako ni bora kuliko kile unachotamani kwenye maisha ya wengine.
 12. Kununua vitu zaidi hakukuongezei furaha kwa sababu baada ya muda unazoea vile ulivyonunua. Furaha inatokana na yale unayofanya kwenye maisha, siyo unayomiliki. Hivyo wekeza kwenye yale unayofanya zaidi kuliko kununua vitu zaidi.
 13. Inapokuja upande wa fedha, kuwa na kiasi cha fedha kitakachokuwezesha kuendesha maisha yako bila ya kutegemea kipato cha moja kwa moja, usijilinganishe na yeyote kifedha na hata kama una fedha nyingi kiasi gani, ishi maisha ya kawaida, utajiri hujenga wivu.
 14. Jiwekee ukomo kwenye vitu utakavyojihusisha navyo, jua ni maeneo gani uko vizuri na weka juhudi kwenye hayo, mengine yote achana nayo. Huhitaji kufanya kila kitu ndiyo ufanikiwe, unahitaji kufanya machache kwa ubora.
 15. Ung’ang’anizi ni muhimu sana, hakuna kizuri kinachotokea haraka, inahitaji muda na jitihada. Ukishachagua maeneo muhimu kwako, kinachofuata ni kazi na kujipa muda. Usihangaike na njia za mkato.
 16. Usijiweke kwenye gereza la wito, usilazimishe kufanya kitu kwa sababu unafikiri ndicho unapaswa kufanya kwenye maisha yako. Fanya kile unachoweza kufanya na kifanye vizuri, huku ukikazana kuwa bora zaidi.
 17. Kama unafanya vitu ili wengine wakuone na kukusifia, utaishia kuwa mtumwa wa wengine. Acha kupima umuhimu wako kwa namna wengine wanavyokuchukulia, fanya kile kilicho sahihi kwako na usijali wengine wanasema au kuchukuliaje.
 18. Unaweza kujibadilisha wewe mwenyewe, lakini huwezi kumbadili mtu yeyote. Hivyo acha kukazana kuwabadilisha watu, chagua kujihusisha na watu ambao tayari unaendana nao ambao huhitaji mabadiliko yoyote kwao, badala ya kuhangaika kuwabadili watu, utachoka na hutafanikiwa.
 19. Jiwekee malengo ambayo unaweza kuyafanyia kazi wewe kulingana na unachotaka na uwezo ulionao. Achana na malengo ambayo yanategemea namna gani wengine wanafanya, kujiwekea malengo kama kutaka kuibadili dunia ni kujiandaa kushindwa.
 20. Ndani yako kuna nafasi mbili, kuna nafsi ambayo ipo kwenye wakati uliopo na kuna nafsi ambayo ipo kwenye wakati uliopita. Nafsi iliyopo kwenye wakati uliopo ndiyo inayopima kile unachofanya sasa, na nafsi iliyopo kwenye wakati uliopita ndiyo inakupa uzoefu. Zote ni muhimu, unapaswa kujua wakati gani wa kuzitumia.
 21. Ishi kwenye wakati uliopo, weka mawazo yako yote kwenye kile unachofanya sasa, kwa njia hii utaongeza umakini na utafurahia chochote unachofanya.
 22. Hadithi nyingi unazojiambia kuhusu maisha yako siyo sahihi, ni uongo unaojipa ili usione uhalisia wa maisha yako. Ili kuwa na maisha bora, unahitaji kuvuka uongo huo na kujiambia hadithi sahihi ya maisha yako, kuanzia wewe ni nani, unataka nini na unafanya nini.
 23. Siku utakayokufa huenda hutajijua kama hata unakufa, lakini wote tuna uhakika kwamba siku moja tutakufa. Na hapa wengi huwa tunajidanganya kwamba tunataka kuwa na kifo kizuri. Badala ya kuhangaika na kutafuta kifo kizuri, kazana kuishi sasa, tumia muda ulionao kuishi vizuri, na kifo kitakukuta, kwa namna kitakavyokukuta.
 24. Kujikumbusha makosa uliyofanya nyuma na kuyajutia, kujikumbusha waliokuumiza na kuwalalamikia ni kupoteza muda wako na maisha yako pia. Jifunze kwa yaliyopita, lakini ishi leo, kwa kufanya kilicho bora leo, usijilaumu kwa yaliyopita wala kumlaumu yeyote kwa kilichotokea huko nyuma.
 25. Vitu tunavyofanya kwenye maisha yetu vina pande mbili; raha na maana. Tunasukumwa kufanya vitu kwa sababu labda vina raha kwetu kufanya au vina maana kwetu. Maisha bora ni kufanya vitu ambavyo vina raha na maana na siyo kuegemea upande mmoja pekee.
 26. Jiwekee misingi ambayo utaisimamia na kuiishi kwenye maisha yako, na hutaivunja hata kama inagharimu maisha yako. Kuwa na misingi ambayo hutaivunja hata kama itakugharimu kufa, na hii itafanya maisha yako kuwa rahisi.
 27. Watu watakapokushambulia ili uvunje misingi yako, na wengi watafanya hivyo, kuwa imara na usianguke. Watu watasema mengi kuhusu misingi yako, lakini simama imara, usijaribu hata mara moja kuvunja misingi yako ili kukubaliana na mtu, kwa njia hiyo utaendelea kuvunja misingi yako na maisha yatakosa maana.
 28. Inapokuja kwenye misingi yako, usiruhusu uwanja wa majadiliano, kama ni hapana ni hapana, hakuna haja ya kujadiliana namna gani ya kuifanya hapana hiyo iwe rahisi zaidi. Hata kama unaambiwa hii ni tofauti au kuna faida kubwa, au ukapewa fedha nyingi, hapana inabaki kuwa hapana.
 29. Kuwa na kitabu cha kuandika hofu zako, unapokuwa na kitu chochote kinachokupa hofu au wasiwasi, kiandike kwenye kitabu hicho. Kwa kujua umeandika, akili yako itaacha kuwa na hofu au wasiwasi na utaweza kufikiria yale muhimu. Ukishaandika hofu hizo, jiulize kama ipo ndani yako kuchukua hatua au ipo nje ya uwezo wako na kukubaliana nazo au kupuuza.
 30. Akili zetu ni volkano ya maoni, tunapenda kuwa na maoni kwenye kila kinachotokea. Lakini maoni mengi huwa siyo sahihi, kwa sababu hatuna utaalamu wa yale tunayotolea maoni. Maisha yako yatakuwa bora kama utakuwa na maoni machache, na tena kwenye yale maeneo ambayo una ubobezi. Kwenye maeneo mengine, usiogope kusema huna maoni.
 31. Jenga wigo wako kiakili, ambao utaweza kukukinga na chochote kitakachotokea. Jua ya kwamba, chochote ulichonacho sasa, kinaweza kuondoka muda wowote, hivyo usiweke uhakika wako kwenye vitu au vitu, bali ndani yako, ndani ya uwezo wako.
 32. Kuondokana na wivu, usijilinganishe na yeyote, pia kubali kwamba kuna watu watakaokuwa wamekuzidi kwa chochote unachofikiri upo juu. Pia kuwa makini na mitandao ya kijamii, sehemu kubwa ya maisha ambayo watu wanaonesha kwenye mitandao ya kijamii siyo halisi.
 33. Kuzuia tatizo lisitokee ni rahisi na bora kuliko kutatua tatizo ambalo limeshatokea. Hivyo weka juhudi zako kuzuia matatizo kabla hayajatokea na hutasumbuka na matatizo ambayo yameshatokea.
 34. Jipumzishe na matatizo ya dunia. Kuna mambo mengi sana mabaya yanayoendelea kwenye dunia, vita, mauaji, ugaidi, njaa na kadhalika. Yote haya yanaumiza sana kuyafikiria. Lakini hakuna kikubwa unachoweza kufanya kuyatatua, hivyo badala ya kuyafikiria na kujipa mzigo, tua mzigo huo. Jua kuna mabaya yanaendelea kwenye dunia, lakini kazana kuifanya kazi yako wewe vizuri, hii ndiyo njia bora kabisa kwako kuisaidia dunia.
 35. Kuna rasilimali tatu muhimu sana kwenye maisha yako, umakini, muda na fedha. Muda na fedha kila mtu anajua njia bora ya kusimamia, lakini umakini ndiyo una changamoto, hasa kwenye zama hizi za taarifa na mitandao ya kijamii. Chunga sana umakini wako, chuja sana kila aina ya taarifa unayopokea na mawazo yanayoingia kwenye akili yako. Weka umakini wako wote kwenye kile unachofanya.
 36. Soma kidogo, lakini soma mara mbili. Sehemu kubwa ya vitabu unavyosoma utasahau kabisa na huenda hutakumbuka hata kitabu kilihusu nini. Unapokuwa kijana soma vitabu vingi uwezavyo, usichague, wewe soma. Lakini kadiri umri unavyokwenda anza kuchagua vitabu vya aina gani unasoma. Soma vitabu vichache, lakini visome mara mbili. Chagua vitabu vyako kama 100 ambavyo utavisoma kwa kurudia rudia ndani ya miaka 10 na utajifunza mengi na kuweza kuwa bora zaidi.
 37. Epuka kufuata itikadi yoyote ile, kuwa huru kwenye fikra zako na fanya maamuzi kulingana na fikra zako. Usifuate itikadi na kuzitumia kufanya maamuzi, utafanya makosa mengi kwa sababu itikadi zimetengenezwa kwa makusudi fulani na hivyo haziwezi kutumika kwenye maeneo yote.
 38. Wakati mwingine utaona thamani ya maisha kwa kujaribu kuondoa vitu fulani. Unaweza kuona mtu fulani ni kero kwako, lakini jiulize kama asingekuwepo kabisa, maisha yako yangeendaje? Huwa tunachukulia vitu kwa ukawaida mpaka pale tunapovikosa ndiyo tunajutia. Kabla hujakikosa kitu, fanya zoezi la kuchukulia kama kitu hicho hakipo na utaona thamani yake.
 39. Kadiri unavyotumia muda mwingi kufikiria na kutafakari jambo, ndivyo inavyokuwa vigumu kwako kuchukua hatua. Hivyo jifunze kufikia maamuzi haraka, kisha ukishaamua, chukua hatua, usianze tena kufikiria na kutafakari. Utajifunza mengi kwa kuchukua hatua kuliko kwa kufikiria na kutafakari.
 40. Ili kuweza kuelewana na wengine, jaribu kuvaa viatu vyao na kutembea kwenye viatu hivyo. Jiweke kwenye nafasi ya wengine na kufikiri au kufanya kwa namna wanavyofanya wao, na utaelewa kwa nini wanafanya kile wanachofanya.
 41. Mabadiliko makubwa yanayotokea kwenye dunia yanatokea kwa sababu wakati umefika na siyo kwa sababu watu fulani wameyasababisha. Huwa tunapenda kuwahusisha watu na mabadiliko makubwa, tukifikiri bila wao mabadiliko yasingetokea. Tuchukue mfano rahisi, kwa mfano kama Nyerere hakupigania uhuru wa Tanzania, je unafikiri mpaka sasa Tanzania ingekua kwenye utumwa? Jibu ni hapana, ingepata uhuru kupitia mtu mwingine.
 42. Sehemu pekee unayoweza kuleta mabadiliko makubwa ni kwenye maisha yako binafsi, kazana na hilo na utaweza kuwa na maisha bora. jua kwamba mengine yoyote unayoweza kuwa unajisumbua nayo yapo nje ya uwezo wako, na kama unataka kujipima kwa jinsi unavyoweza kubadili mengine, unajiweka kwenye nafasi ya kushindwa.
 43. Dunia haipo sawa, na wala dunia haiendi kulingana na mpango wako wa usawa ulionao. Dunia inaenda kama inavyoenda, kulingana na mipango yake yenyewe. Kuna mambo yatakayotokea ambayo siyo sawa kabisa kwako, lakini haitakusaidia kwa kuilaumu dunia. Badala yake ni kupokea na kusonga mbele.
 44. Watu wengi wamekuwa wanaiga tabia za watu waliofanikiwa, lakini wanaishia kwenye kuiga tabia na hawazalishi chochote. Usiwe mtu wa kuiga tu tabia, badala yake kuwa mtu wa kutoa matokeo. Maisha siyo maigizo, maisha ni kile unachofanya.
 45. Ili kufanikiwa huhitaji kufanya kila kitu au kujua kila kitu. Badala yake chagua eneo lako ambalo unaweza kufanya vizuri, kisha kazana kufanya vizuri, kuwa bora kuliko wengine wote na utaweza kufanikiwa zaidi. Kadiri unavyochagua vizuri eneo lako na kuweka juhudi kubwa, ndivyo unavyotumia nguvu zako na umakini wako vizuri.
 46. Usishindane na yeyote, kimbia mbio zako mwenyewe. Na ili kufanikiwa, epuka maeneo yenye ushindani mkali, kwa kuwa na kitu cha kukutofautisha wewe na wengine, ambacho hakuna mwingine anayeweza kuwa nacho ila wewe.
 47. Kwenye jamii kuna makundi mbalimbali, ukiwa ndani ya kundi unapaswa kufanya kama kundi linavyotaka, lakini pia unakosa uhuru fulani wa kufanya unavyotaka mwenyewe. Ukiwa nje ya kundi, unaweza kufanya unavyotaka mwenyewe, lakini unakosa manufaa fulani ya kuwa ndani ya kundi. Suluhisho ni kuwa mguu mmoja ndani ya kundi na mguu mwingine nje. Kuwa ndani ya kundi, lakini kuruhusu akili yako ifikiri kama walio nje ya kundi.
 48. Ili kupata watu sahihi, utahitaji kupitia watu wengi ambao siyo sahihi, ili kujua nini hasa unataka na maisha yako, unahitaji kufanya mengi. Kadiri unavyokutana na vitu vingi, ndivyo unajifunza jinsi ya kufanya maamuzi ya kipi sahihi kwako.
 49. Kadiri unavyokuwa na matarajio machache, ndivyo unavyokuwa na furaha kubwa. Matarajio makubwa ni chanzo cha kukosa furaha kwa wengi, hasa pale matarajio hayo yanapokuwa nje ya uwezo wao. Kuwa na malengo ya maisha yako, weka juhudi kubwa kwenye kuyafikia, lakini kuwa tayari kupokea matokeo yoyote, mazuri au mabaya.
 50. Jifunze kutofautisha kati ya mawazo na mawazo mazuri, bidhaa na bidhaa bora, uwekezaji na uwekezaji mzuri. Asilimia 90 ya vitu vyote unavyokutana navyo, siyo muhimu, yaani ukiachana navyo hutakosa chochote. Ni asilimia 10 tu ndiyo muhimu, jua hiyo asilimia kumi na ukazane nayo huku ukipuuza mengine yote.
 51. Kuwa na kiasi, haijalishi umefanikiwa kiasi gani, miaka 200 ijayo, huenda hakuna atakayejua hata kama uliishi hapa duniani. Kila unapoanza kujiona wewe ni muhimu kuliko wengine, kumbuka kitakachotokea miaka 200 ijayo, dunia itakuwa imekusahau kabisa. Ishi maisha yenye maana kwako na siyo maisha ya kujionesha na kutaka wengine waone wewe ni muhimu kuliko wao.
 52. Kuna orodha nyingi za watu waliofanikiwa, kuanzia ndani ya nchi mpaka dunia nzima. Lakini jinsi mafanikio hayo yanavyopimwa inaweza isiwe sahihi kwako. Mafanikio ya kweli kwako ni mafanikio ya ndani yako, ambayo siyo rahisi kupimwa kwa nje. Mafanikio ya ndani utayapata kwa kuweka juhudi kwenye yale maeneo uliyochagua, kuweka umakini wako kwenye mambo yaliyo ndani ya uwezo wako na kuachana na mengine yote. fedha, madaraka na umaarufu ni vitu vya nje, ambavyo huwezi kuvidhibiti, unachoweza kudhibiti ni hatua unazochukua. Kazana kuwa bora kila siku na weka juhudi zaidi kwenye kile ulichochagua kufanya.

Rafiki, hizo ndiyo njia 52 za kuwa na maisha mazuri, maisha yenye maana kwako, maisha yenye furaha na mafanikio makubwa. Zipo njia nyingi zaidi, lakini hizi 52 zitakupa mahali pa kuanzia.

Na kama unapenda kujifunza falsafa itakayokuwezesha kuendesha maisha yako kwa misingi bora, ambayo haitetereshwi na chochote, karibu kwenye KISIMA CHA MAARIFA ujifunze falsafa ya Ustoa.

#2 MAKALA YA WIKI; CHANGAMOTO 10 TUTAKAZOTATUA KWENYE SEMINA.

Rafiki, juma hili nilikushirikisha makala ya changamoto 10 tunazokwenda kufanyia kazi kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, ni changamoto ambazo zinawagusa wengi, na huenda na wewe zinakugusa pia.

Soma makala hiyo hapa, na kama changamoto hizo zinakugusa basi karibu sana kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018; Changamoto 10 Tutakazofanyia Kazi Kwenye Semina Ya Kisima Cha Maarifa 2018.

Pia nilikushirikisha makala kuhusu faida tano za kushiriki semina inayofanyika moja kwa moja, ambazo huwezi kuzipata kwa kujisomea mwenyewe au kushiriki semina ya mtandaoni. Zisome faida hizo hapa; Hizi Ndizo Faida Tano (05) Za Ziada Utakazopata Kwa Kuhudhuria Semina Ya Moja Kwa Moja, Ambazo Huwezi Kuzipata Kwa Kujisomea Mwenyewe.

#3 TUONGEE PESA; USIKUBALI KUPOTEZA FEDHA KUKUVURUGE.

Rafiki, kwenye njia 52 nilizokushirikisha za kuwa na maisha mazuri, njia ya kwanza kabisa mwandishi amezungumzia kuhusu dhana anayoiita MENTAL ACCOUNTING, yaani kuwa na uhasibu wa kifikra. Hapa mwandishi anatufundisha jinsi ya kugeuza upotevu wa fedha kuwa ushindi kwetu.

Na kuna mfano mzuri sana aliotumia, ambao nimejikuta nilikuwa nautumia bila hata ya kuwa nimejua dhana hii.

Kuna wakati unaweza kuwa unaendesha gari, ukakutana na askari wa usalama barabarani, ambaye anakuwa kama amejipanga kuhakikisha kwamba anapata kosa kwako na kukupiga faini au kutaka umpe rushwa ili asikuandikie faini.

Sasa kwangu kutoa rushwa kwa kosa la kulazimishiwa nimekuwa sijisikii vizuri. Hivyo nimekuwa najaribu kutaka kupata ufafanuzi zaidi na kwa nini ni lazima iwe faini. Na ikitokea hakuna mabadiliko, basi huwa namwambia askari aniandikie faini na nitailipa. Sasa wengi hushangaa kwa nini ukubali kulipa elfu 30 ya faini wakati unaweza kutoa rushwa labda ya shilingi elfu kumi na usipigwe faini, ukaokoa elfu 20?

Hivi ndivyo ambavyo nimekuwa nawaza, nikiandikiwa faini ya elfu 30, nailipa moja kwa moja serikalini, hivyo nachukulia kama ni sehemu ya kulipa kodi, ambayo ndiyo inatumika kufanya maisha kuwa bora zaidi kwa wananchi, kwa utoaji wa huduma bora za afya, elimu na kadhalika. Lakini kama nitampa askari rushwa, huenda ataenda kuitumia vibaya, labda kulewa au mengine, ambayo hayatakuwa na manufaa kwa yeyote.

Hivyo nimekuwa najikuta napokea faini bila ya shida yoyote, kwa sababu najua ni sehemu ya mchango wangu kwa serikali.

Kama unataka kupotea kwa fedha ndogo ndogo kusiwe kikwazo kwako, basi chukulia fedha inayopotea kama sadaka umetoa au kama msaada kwa wasiojiweza.

Mwandishi pia anashauri uwe na mfuko wa kiasi cha fedha unachopanga kutoa kila mwaka kama sadaka au msaada. Kisha kila fedha unayopoteza, kwa namna ambayo usingeweza kuiokoa, uiingize kwenye mfuko huo na utakuwa na amani linapokuja swala la fedha.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; MAANDALIZI YA SEMINA YANAKWENDA VIZURI SANA.

Rafiki yangu mpendwa, kama ambavyo nimekuwa nakuambia kwa muda sasa, SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018 itafanyika jumamosi ya tarehe 03/11/2018. Maandalizi ya semina hii yanakwenda vizuri sana na tumeshafikia makubaliano mzuri na hoteli ambapo itafanyika semina hii.

Huduma zote muhimu zitapatikana kwa ubora wa hali ya juu sana, hivyo kazi ni kwako kufanya malipo kabla ya tarehe 31/10/2018 ili uweze kushiriki semina hii ya kipekee sana kwetu kwa mafanikio yetu.

Ada ya kushiriki semina hii ni tsh 100,000/= (laki moja) ambayo inajumuisha huduma zote za siku ya semina, kuanzia chai, chakula vinjwaji, vijitabu vya kuandikia, kalamu na kadhalika.

Nafasi za kushiriki semina hii ni 100 pekee, na watu waliodhibitisha kushiriki mpaka sasa ni 110. Hivyo nafasi zitatolewa kwa wale wanaowahi kulipia ada ya semina.

Mwisho wa kulipa ada ni tarehe 31/10/2018, hivyo kama hutaki kukosa nafasi hii, lipa ada yako mapema.

Namba za kufanya malipo ni 0755 953 887 au 0717 396 253 majina ya namba hizo ni AMANI MAKIRITA.

Karibu sana kwenye semina ya KISIMA CHA MAARIFA 2018, tujifunze na kupata hamasa ya kuchukua hatua kwa mwaka mzima bila ya kuchoka.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; USHINDI MKUBWA KWENYE DUNIA TUNAYOISHI SASA.

“To be yourself in a world that is constantly trying to make you something else is the greatest accomplishment.” – Ralph Waldo Emerson

Changamoto kubwa sana ya zama tunazoishi sasa ni dunia kutaka uwe kwa namna fulani, ambayo ni tofauti na wewe. Ni vigumu sana kuwa wewe kwenye dunia tunayoishi sasa. Tembelea mitandao ya kijamii na utajionea jinsi ambavyo dunia inakulazimisha uwe wa namna fulani. Fuatilia habari mbalimbali na utaona namna ambavyo kila mtu ana cha kukuambia kuhusu ufanye nini na maisha yako.

Unahitaji ujasiri mkubwa sana wa kukataa ushawishi huu wa dunia na kusimama mwenyewe, kuishi maisha yako, kuwa wewe. utapingwa, utakatishwa tamaa na utarushiwa kila aina ya maneno, kama haupo imara na kama hujajitoa hasa, hutaweza kufika mbali.

Nakutakia kila la kheri kwenye juma unalokwenda kuanza rafiki, liwe juma bora sana kwako, juma la kuishi maisha mazuri kwako na kukazana kuwa wewe. Pia usichelewe kulipa ada ya kushiriki SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018 kama bado hujafanya hivyo.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu