Kwa chochote unachochagua kufanya kwenye maisha yako, watu hawatakaa kimya, kila mtu atakuwa na lake la kusema.

Wapo ambao watakuunga mkono na kukupa moyo wa kuendelea kufanya.

Lakini wapo ambao watakukatisha tamaa na kukuzuia usiendelee kufanya.

Unapokuwa unaanza kufanya kitu, ukiwa bado hujapata uzoefu na unapokutana na changamoto, unaweza kujikuta kwenye wakati mgumu sana. Ukashindwa kujua ni watu gani sahihi kwako kuwasikiliza.

Kwa sababu unapokutana na changamoto, wote utawaona wapo sahihi, na huenda wale wanaokukatisha tamaa, wataonekana wapo sahihi kuliko wale wanaokupa moyo. Wale wanaokuambia tumeona wengi kama wewe walioshindwa, wataonekana wapo sahihi sana.

Swali ni je ni watu gani sahihi kwako kuwasikiliza? Je inabidi uwasikilize wale wanaokupa moyo au wanaokukatisha tamaa.

Kwa hali ya kawaida utajiambia uwasikilize wote, ili hata kama unaendelea ujue mambo gani ya kuwa makini nayo.

Lakini mimi nakuambia kitu kimoja, wasikilize wale wanaopata matokeo unayotaka kuyapata. Kama mtu hapati matokeo unayotaka kuyapata, kama mtu hafanikiwi kama unavyotaka kufanikiwa, anakosa sifa ya wewe kumsikiliza.

Kwa msimamo huu, utawaepuka wengi, wenye ushauri mbaya na hata mzuri pia, lakini utaweka umakini wako kwa mtu sahihi kwako, ambaye una mengi ya kujifunza kwake.

Kwa msimamo huu pia wengi wataona una dharau na hujali, lakini hupaswi kujali kumsikiliza mtu ambaye hazalishi matokeo.

Rafiki, kuongea ni rahisi, kushauri ni rahisi, lakini kufanya ni kugumu. Kufanya kuna changamoto nyingi sana na ukiona mtu anapata matokeo mazuri, basi jua kuna namna tofauti anafanya na ameweza kuvuka vikwazo vingi.

Huyo ndiyo mtu sahihi wa kumsikiliza, kwa sababu hata kama atakukatisha tamaa, atakushirikisha uzoefu aliopitia yeye, ambao utakupa funzo kubwa.

Na kama mtu anazalisha matokeo, hawezi kuwa hasi hata kidogo, maana angekuwa hasi asingefika pale alipofika. Hivyo ukiona mtu anazalisha matokeo unayotaka lakini yupo hasi, chunguza kwa umakini, kuna kitu kitakuwa hakipo sawa mahali, labda anadanganya kuhusu matokeo yake au kuna namna amepita njia zisizo sahihi, ambazo hataki wengine wazijue.

Rafiki, unapojikuta njia panda kwa watu gani uwasikilize, angalia kwanza matokeo wanayoyatengeneza. Kama mtu hapati matokeo unayotaka kupata, huna haja ya kumsikiliza. Tena kama ndiyo anakukatisha tamaa, unapaswa kumpuuza mara moja.

Waongeaji ni wengi, watoaji wa ushauri wa bure ni wengi, wanaojifanya kuwa wanajua sana ni wengi, lakini wanaopata matokeo halisi ni wachache sana. Hawa ndiyo wa kukazana nao, maana ndiyo watakaokupa ushauri na maelekezo sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha