Siri za mafanikio na tabia za mafanikio ni maeneo ambayo yanashamiri sana zama hizi kwenye uandishi na mafunzo mbalimbali. Kwa kuwa mafanikio yana kanuni zake, fikra zetu ni kwamba kama tutafanya kile ambacho watu waliofanikiwa wamefanya, basi na sisi pia tutafanikiwa.

Na hili limewafanya wengi kutafuta siri zaidi, kutaka kujua kila aina ya tabia ambayo watu waliofanikiwa wanayo. Hapa wengi wamekuwa wanataka kujua kile wanachofanya waliofanikiwa, kuanzia wanapoamka mpaka wanapolala, wanataka kujua mpaka wanachokula na wanachokunywa.

Ni kweli kwamba kile wanachofanya waliofanikiwa kina mchango kwenye mafanikio yao, lakini kinaweza kisiwe na mchango kwenye mafanikio yako.

Iko hivi rafiki, kitu kimoja pekee ambacho watu wote waliofanikiwa wanacho, ni mafanikio. Vingine vyote wanatofautiana sana.

Utakuta watu wawili waliofanikiwa sana, lakini tabia zao ni tofauti kabisa, utakuta wanayofanya yanatofautiana, lakini wote wamefanikiwa.

Hivyo kwa kufuatilia tabia na siri za mafanikio ya wengine, utafika mahali na kuona kama vitu vinaanza kupingana, unaanza kuona watu wanafanya vitu vinavyopingana, lakini bado wote wamefanikiwa.

Ili kujiepusha na hali hii ya kuwa njia panda, hasa pale yale unayojifunza yanapopingana, unahitaji kujua kwamba hakuna tabia moja au kitu kimoja kinachoweza kuleta matokeo kwa kila mtu.

Muhimu zaidi, unahitaji kujijua wewe mwenyewe kwanza, kujua uwezo uliopo ndani yako, kujua maeneo gani upo imara na maeneo gani una madhaifu. Unahitaji kujua nini hasa unachotaka na maisha yako, mafanikio kwako ni nini na utajuaje kwamba umefanikiwa.

Ukishajijua na kujua unataka nini, sasa unapaswa kuwachagua watu wachache ambao unakwenda kujifunza kwao. Watu hawa wanakuwa wanaendana na kile unachotaka wewe, hivyo mafunzo yao yanakuwa yanaendana na siyo kupingana yenyewe au kupingana na kile unachoamini wewe.

Kadiri unavyochagua watu wachache, au hata kuchagua mtu mmoja wa kujifunza kwake, na ukajifunza kila kitu kutoka kwake, kisha ukachukua hatua, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi ya kufanikiwa zaidi.

Nikukumbushe kwamba wakati unafuata wale wachache uliowachagua, siri na tabia za wengine hazitaacha kukuvutia, tena siri na tabia zinazopingana na zile ulizochagua kuishi. Hivyo unapaswa kuwa tayari kuepuka ushawishi utakaoupata kwa kutaka kuiga ya wengine, ambayo hayaendani na unachotaka au unachoamini.

Jua kuna tofauti kubwa sana baina ya waliofanikiwa, kuanzia mtazamo, tabia na hata yale wanayofanya. Hivyo jijue wewe mwenyewe kwanza kabla hujachagua ni watu gani waliofanikiwa ambao utajifunza kutoka kwao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha