Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari ANDIKA MAHALI…
Pamoja na mapinduzi makubwa ya teknolojia ambayo yanaendelea kutokea hapa duniani, ipo teknolojia moja ya zamani sana ambayo ina manufaa makubwa sana kwetu.
Teknolojia hiyo ni kuandika kwa kitumia kalamu na karatasi.
Ni rahisi sasa kaundika kwenye simu na hata kompyuta,
Ni rahisi hata kurekodi sauti na hata video,
Lakini teknolojia yenye nguvu sana kwetu ni kuandika kwa kalamu na karatasi.

Unapoandika chochote kwa kalamu na karatasi, unakuwa umejitoa zaidi kwa ajili ya kitu hicho.
Unapoandika kwa kalamu na karatasi, unaiambia akili yako kwamba hicho ulichoandika ni muhimu sana.
Unapoandika kwa kalamu na karatasi ni kama unajiwekea mkataba kwenye kile ulichoandika, hivyo unasukumwa kukitekeleza.

Hivyo mwanamafanikio, chochote ambacho ni muhimu zaidi kwako, chukua muda na andika kwa kalamu na karatasi, siyo kwa kuchapa au kusema, bali kwa kuchora maandishi kwa mikono yako.
Mara zote kuwa na kijitabu na kalamu, ambavyo utavitumia kwa kuandika.

Na yafuatayo ni mambo muhimu kwako kuyaandika kila siku kwa kalamu na karatasi.
Moja; andika maono, ndoto, malengo na mipango yako ya muda mfupi na muda mrefu. Andika haya kila siku, unakuwa unaikumbusha akili yako na kujiweka zaidi kuhakikisha unatekeleza mipango hiyo.
Mbili; andika yale uliyopanga kufanya kwenye siku yako, kuwa na orodha ya vitu vya kufanya, na fuata orodha hiyo. Bila orodha itakuwa vigumu sana kutekeleza chochote.
Tatu; andika orodha ya vitu ambavyo hutafanya, hii ni orodha muhimu sana kukusaidia wewe usipoteze muda kwa mambo yasiyo muhimu.
Nne; andika hofu na wasiwasi wowote ulionao, kwa kufanya hivi u aipumzisha akili na kuipa nafasi ya kufikiria yale muhimu zaidi.
Tano; andika mawazo mapya unayokutana nayo kwenye siku yako, kwa njia hii hutayasahau.

Ukawe na siku bora sana ya leo mwanamafanikiom siku ya kutumia teknolojia ya kuandika kwa kalamu na karatasi ili kuweza kufanya yale muhimu sana.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha