As Rilke wrote, “Time does not ‘console’ as people say superficially; at best it puts things in their place and it creates order.”
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari MUDA SIYO TIBA, BALI UNAWEKA VITU SAWA…
Tumezoea kutumia kauli kwamba muda ni tiba ya kila kitu.
Pale kitu chochote kinapotushinda au kinapokuwa kikubwa sana kwetu na kushindwa kutatua, basi tunaachia muda ufanye kazi yake.
Ni kweli kadiri muda unavyokwenda, ndivyo yale yaliyotushinda yanavyoacha kuwa tatizo kwetu.
Na hii inatokea siyo kwa sababu muda umeyabadili mambo hayo, bali kwa sababu muda unavyokwenda, vitu vinakaa sawa.
Pale kinapotokea kitu ambacho hatutegemei, au kitu tunachofanyia kazi kinatushinda, huwa hatukubali kirahisi.
Badala yake tunakataa ndani yetu, na wakati mwingine tunaona labda tunaonewa au kwa nini itokee kwetu tu.
Kile kinachotokea kinakuwa kimeibua hisia zetu na hivyo hatufikiri wala kuona sawasawa.
Lakini kadiri muda unavyoenda, hisia zilizoibuka zinatulia, tunapata nafasi ya kuangalia jambo hilo vizuri na kufikiri kwa kina. Na hapo tunaanza kuona kwamba ni sehemu ya maisha kukutana na mambo kama hayo.
Pia kadiri muda unavyoenda wengine wanapatwa na mambo makubwa au magumu kuliko yaliyotupata sisi, kiasi kwamba tunaona ya kwetu yalikuwa madogo na ya kawaida sana.
Pia muda unatupa utulivu wa kufikiri kwa kina na kwa njia hiyo tunaweza kupata suluhisho la kilichoonekana ni kigumu kwetu.
Hivi ndivyo muda unavyotusaidia kwa yoyote magumu tunayokutana nayo. Siyo kwa kuyatatua, bali kwa kuweka mambo sawa, na mambo yakishakaa sawa, ni rahisi kutatua au kuachana na kinachokusumbua.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuutumia muda kuweka mambo sawa, hasa pale unapokutana na magumu kwenye maisha yako.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha