Watu waliofanikiwa sana, mara zote huwa wana kitu cha kufanya.

Huwezi kuwakuta wamekaa na kujiuliza sasa nifanye nini.

Au wakajiambia wanapoteza muda kidogo kwa kufanya mambo yasiyo muhimu huku wakifikiria wafanye nini.

Siku ya wale waliofanikiwa huwa imejaa, tangu kuamka mpaka wanaporudi kulala.

Lakini siku ya wale ambao hawajafanikiwa, ipo tupu kabisa. Wana muda mwingi kuliko wanavyoweza kuutumia, hivyo wanaupotezea kwenye mitandao ya kijamii, kufuatilia maisha ya wengine, kufuatilia habari na hata kuharibu afya zao kwa vilevi na mengine kama hayo.

Mpigie simu mtu ambaye hajafanikiwa muda wowote na atapokea na kuwa tayari kuongea hata kama huna jambo la muhimu la kuongea. Ni kama vile alikuwa anasubiri simu yako na hana kikubwa alichokuwa anafanya, ambacho ni muhimu kuliko simu ambayo nayo haina umuhimu.

Mwambie mtu asiyefanikiwa kwamba unahitaji muda wake, labda muende mahali na atakuwa tayari, bila ya kipingamizi chochote. Na hapo utaona wazi kwa nini watu ambao hawajafanikiwa inakuwa vigumu kwao kufanikiwa.

Kama bado upo kwenye kundi la wasiofanikiwa, na unataka sana kufanikiwa, kitu cha kwanza kufanya ni kuijaza kalenda yako ya siku, kwa siku nzima. Kila saa na kila dakika ya siku, pangilia kitu utakachokuwa unakifanya, na kifanye kama ulivyopangilia.

Usiwe na dakika kwenye siku yako unazojiuliza ufanye nini, au kujiambia acha nipoteze muda kidogo. Unapaswa kuwa na kalenda iliyojaa, maana wanasema kalenda yako ikiwa wazi unakaribisha matatizo.

Kuwa bahili wa muda wako, utoe kwa uchoyo sana, na kwa ugumu sana na utoe kwa wale tu ambao wanastahili, wale ambao wana umuhimu na wana cha kuchangia kufika kule unakotaka kufika.

Neno lako la kwanza linapaswa kuwa hapana, pale mtu anapokuwa anataka muda wako, au umakini wako au nguvu zako. Halafu mtu anapaswa kukushawishi kwa nini ubadili hapana yako kuwa ndiyo. Kama huwezi kusema neno hapana, hasa kwa vitu ulivyozoea, ambavyo havina umuhimu mkubwa kwako, utaendelea kushangaa mbona muda wako unaisha na huoni ambacho umefanya.

Mara zote kuwa na kitu cha kufanya, na mara zote tumia muda wako kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwako.

Na hii haimaanishi kwamba utakuwa unafanya kazi muda wote bila ya kupumzika, bali kwenye ratiba yako, unatenga muda wa kupumzika, na muda huo unapofika, unapumzika kweli.

Fanya kila kitu kwa mpangilio mzuri kwenye maisha yako na utaweza kuona faida ya muda na nguvu zako kwenye maisha yako. Lakini kama utataka kupelekwa pelekwa tu na kila kinachotokea, usimlaumu yeyote pale muda unapokwenda na usione chochote kikubwa ulichofanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha