Tofauti kubwa kati ya wale wanaofanikiwa na wanaoshindwa huwa haianzii kwenye akili, bali kwenye nguvu.
Kuna kiwango fulani cha akili ukishakuwa nacho, basi kinatosha kwa mafanikio yako na hata mwenye akili kuliko wewe, hawezi kukushinda kwa sababu tu ya akili yake.
Kwa mfano kama unaweza kusoma hapa, hii ina maana kwamba unajua kusoma na kuandika, unaweza kutumia simu au kompyuta na unaweza kutumia teknolojia kama ya mtandao wa intaneti mpaka umeweza kupata mafunzo haya.
Ninachotaka kukuambia ni kwamba, kama unaweza kusoma hapa, basi unazo akili za kukutosha kabisa kupata mafanikio makubwa. Unachohitaji sasa ni nguvu zaidi na siyo akili zaidi.
Nguvu ya kuweza kuchukua hatua, bila ya kuchoka, nguvu ya kufanya zaidi, nguvu ya kwenda hatua ya ziada, ni nguvu itakayokuwezesha kufanikiwa zaidi, hata kama huna akili zaidi.
Mafanikio yako ni matokeo ya kuzalisha zaidi, kufanya kazi bora, kutoa huduma bora ambazo watu hawawezi kuzipata kwa wengine. Utaweza kufanya hayo kama utakuwa na nguvu za kutosha.
Akili inakusaidia kuja na mawazo bora, lakini kama tunavyojua, wazo bora linachangia asilimia 1 ya mafanikio, asilimia 99 inachangiwa na jasho, nguvu, juhudi, kuchukua hatua.
Kama mtu anakuzidi kwa akili, wewe mzidi kwa kazi unayoweka, na hiyo itakusaidia sana.
Kwa chochote unachofanya, julikana kama mtu anayefanya kwa ubora wa hali ya juu sana, na siyo kwa maneno bali kwa matendo. Julikana kama mtu ambaye anafanya kazi, na siyo mtu wa maneno na kupoteza muda.
Weka nguvu kwenye kile unachofanya na utaweza kujitofautisha na wengine wote wanaofanya kile unachofanya, hata kama wana akili sana kuliko wewe.
Na ili kuwa na nguvu zaidi unapaswa kuzingatia sana afya yako. Namna unavyokula, mazoezi unayofanya na hata mapumziko unayopata. Unapaswa kuujua vizuri mwili wako na kuusimamia kwa karibu ili wakati wote uwe na nguvu za kuweza kufanya kazi.
Kuamka asubuhi na mapema na kuianza siku yako kabla ya usumbufu wa kelele za dunia itakusaidia kuwa na nguvu zaidi. Kupata chakula bora kwa wakati itakusaidia kuwa na nguvu. Pia kupumzika pale unapokuwa umechoka, unaandaa nguvu zaidi kwa ajili ya baadaye.
Nguvu zako ndiyo kitu kitakachokutofautisha na wengine kwenye mafanikio, na siyo akili kama wengine wanavyofikiri. Akili ni muhimu sana, lakini mchango wake una ukomo, nguvu ni muhimu na mchango wake kwenye mafanikio ni mkubwa na hauna ukomo.
Utengeneze mwili wako kwa namna ambayo utaweza kufanya vizuri kazi zako kwa muda ambao una nguvu za kutosha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,