Rafiki yangu mpendwa,
Hakuna zama ambazo maisha yetu wanadamu yamevurugwa kama zama ambazo tunaishi sasa.
Kwa kipindi kirefu, maisha yetu wanadamu yalikuwa na mpangilio unaoeleweka, watu walikuwa na majukumu wanayoyaelewa na waliyatekeleza kwa kiwango cha juu kwa sababu hawakuwa na namna mbadala.
Miaka 100 iliyopita, kama mtu alikuwa mkulima alilima kwa uwezo wake wote, kwa sababu hakuwa na namna nyingine. Kadhalika kwa wafugaji, wawindaji, waashi, wahunzi na taaluma nyingine chache zilizokuwepo wakati huo.
Maendeleo ya teknolojia yamekuja na kazi nyingi zimerahisishwa sana, kitu ambacho tulitegemea kifanye maisha ya watu kuwa bora zaidi. Lakini matokeo tunayoyaona ni tofauti kabisa. Licha ya maendeleo ya sayansi na teknolojia kurahisisha maisha yetu wanadamu, ubora wa maisha yetu unazidi kushuka chini.
Hii ni kwa sababu kadiri majukumu yetu yanavyokuwa rahisi kufanya, ndivyo tunakuwa na muda mwingi ambao hatuna kazi kubwa ya kufanya na hivyo kutumia muda huo kufanya mambo ambayo siyo mazuri kwetu.
Pia kadiri maendeleo yalivyorahisisha mawasiliano na mwingiliano baina ya jamii tofauti, ndivyo fursa zinavyokuwa nyingi, na kadiri fursa zinavyokuwa nyingi, ndivyo wengi wanavyopoteza muda kwenye kujaribu kila fursa.
Sasa hivi ni vigumu sana kwa mtu kuchagua kitu kimoja au vichache ambavyo atafanya kwa maisha yake yote na kuachana na vingine vyote. Siku hizi watu wanabadilika kama vinyonga. Leo mtu atakuambia fursa hii inalipa sana na anaifanya, kesho anakuambia tayari yupo kwenye fursa nyingine.
Ili kurudisha utulivu kwenye maisha yetu, ili kuweza kutengeneza msingi imara wa mafanikio tunaoweza kuuishi kila siku, kuna mazoezi matano muhimu ambayo nakushauri uyafanye kwenye maisha yako na yatakuwa bora sana.
Mazoezi hayo matano ya kufanya ili kuboresha maisha yako ni kama ifuatavyo;
- Usianze siku yako kwa habari.
Moja ya vitu vinavyowafanya watu waanze siku wakiwa wameshachoka na kukata tamaa, wakiwa wanaona hakuna kikubwa wanachoweza kufanya ni kuanza siku na habari. Waliopo kwenye tasnia ya habari wanajua kwamba mbwa kumng’ata John siyo habari, bali John kumng’ata mbwa ndiyo habari ya kusisimua. Hivyo wanakukusanyia habari zitakazokusisimua, lakini pia zitakuacha ukiwa huna matumaini yoyote mazuri kwenye maisha yako.
Utakusanyiwa habari hasi, za watu walioua au kujiua, watu waliofanya mabaya na utaona picha ya dunia kama vile inazidi kuwa mbaya siku hadi siku. Wakati kuna mambo mengi mazuri sana yanayoendelea duniani na kwenye maisha yako.
Usianze siku yako kwa habari, anza siku yako kwa mipangilio yako na kujifunza yale ambayo ni muhimu zaidi kwa ajili ya mafanikio yako.
- Usiruhusu usumbufu uingilie kile unachofanya.
Usumbufu umekuwa ni kitu cha kawaida sana siku hizi, utakuta mtu anafanya kazi huku simu yake ya mkononi ipi karibu. Ujumbe ukiingia anajibu, simu ikiita anapokea, na mara kwa mara anaacha kazi na kutembelea mitandao ya kijamii ili kuona tu nini kinaendelea. Huwezi kufanya kazi bora kwa kuwa na usumbufu wa aina hii, kazi bora inahitaji utulivu wa akili na kuepuka usumbufu.
Hivyo fanya zoezi la kuondoa usumbufu wakati unafanya kazi ambazo ni muhimu zaidi kwako. Na usumbufu wa kwanza ni simu yako, hivyo unapaswa kuizima au kuiweka kwenye mfumo wa utulivu, kiasi kwamba unaweza kuzama kwenye kazi zako bila ya kusumbuliwa. Pia epuka usumbufu wa wengine kwa kufanya kazi zako eneo ambalo ni tulivu.
- Kuwa pale ulipo, mawazo kwenye kile unachofanya.
Kitu kingine kinachofanya tusifurahie maisha yetu ni mwili kuwa sehemu moja huku mawazo yapo sehemu nyingine. Mwandishi mmoja amewahi kusema watu hawafanyi kazi wala hawapumziki, wapo wapo tu. Mtu akiwa kwenye kazi anafikiria mapumziko, akiwa kwenye mapumziko anafikiria kazi. Hivyo muda wote anakuwa hajielewi nini anafanya na nini anafikiria.
Weka mawazo yako kwenye kile unachofanya, usikubali mawazo yako yaanze kufikiria vitu vingine, hata yanapoenda kwenye vitu vingine, jikumbushe kuyarudisha kwenye kile unachofanya. Kwa sababu hicho ndiyo kitu muhimu zaidi kwako.
Kama kitu hakistahili mawazo yako, basi pia hakistahili kufanya. Na kama unafanya kitu kimoja huku mawazo yapo kwenye kitu kingine, ni bora uache kufanya hicho na ufanye kwanza kile unachokifikiria muda wote, maana kitakuwa muhimu zaidi.
- Weka umakini mkubwa kwenye chochote unachogusa.
Hakuna adui mkubwa wa mafanikio tunayeishi naye sasa kama kukosa umakini. Watu wanafanya vitu kwa mazoea, watu wanafanya vitu wakiwa na haraka na hivyo hawavifanyi kwa ubora au upekee unaostahili. Wanafanya tu ili waonekane amefanya, kitu ambacho hakiwezi kuleta matokeo bora kwa yeyote.
Chochote unachokubali kufanya na muda wako, basi kifanye kwa umakini kweli, weka juhudi zako zote, weka ubunifu wako na kifanye kwa ubora wa hali ya juu sana. Kadiri unavyoweka umakini mkubwa kwenye kile unachofanya, ndivyo unavyotengeneza matokeo mazuri.
- Jipe likizo ya mitandao ya kijamii.
Mitandao ya kijamii imekuwa gereza la watu wengi mno zama hizi. Watu wamekuwa wanafanya vitu ili tu waweke kwenye mitandao ya kijamii. Watu wanaingiza sana maisha kwenye mitandao ya kijamii. Na watu wanaharibu maisha yao kwa kuigiza maisha ya wengine kwenye mitandao hii, wasijue kwamba wanayoiga ni maigizo na siyo maisha halisi.
Unahitaji kujipa likizo ya mitandao ya kijamii, kwa sababu unachopata na unachopoteza haviendani, unapoteza zaidi ya unavyopata kwenye mitandao hii. Unahitaji kujipa likizo kutoka kwenye mitandao hii, unaishi maisha yenye uhalisia kwako na siyo ya maigizo.
Rafiki, haya ndiyo majaribio matano muhimu unayopaswa kuyafanya ili maisha yako yaweze kuwa bora sana.
Lakini pia nimekuandalia siku moja ya kufanya majaribio yote haya, kwa sababu najua peke yako inaweza kuwa shida.
Siku ya SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, tarehe 03/11/2018, itakuwa siku maalumu kwako kufanya majaribio haya matano yote kwa pamoja, kitu ambacho kitakunufaisha sana.
Semina yetu itaanza saa moja kamili asubuhi mpaka saa moja kamili usiku, hii ina maana kwamba kwa masaa 12 utakuwa kwenye semina hii. Sasa nakushauri ufanye majaribio yote hayo matano ndani ya masaa hayo 12 na utanufaika zaidi na semina hii, pia utajijengea uwezo wa kuweza kujisimamia sana.
Hivyo kwenye siku hii ya semina;
Moja; usianze na habari yoyote ile, amka asubuhi na njoo kwenye semina, huhitaji kupata habari nyingine yoyote kwenye siku hiyo.
Mbili; siku hiyo usiruhusu simu iwe usumbufu kwako, zima kabisa simu yako au iweke kwenye utulivu na usiiangalie kila mara. Wajulishe watu wote muhimu kwamba siku hiyo hutapatikana.
Tatu; mawazo yako yote yawe kwenye semina, usianze kufikiria umetoka wapi au umeacha nini, weka mawazo yako pale na jifunze.
Nne; jifunze kwa umakini mkubwa, andika kila unachojifunza, weka mipango kutokana na yale unayojifunza na ondoka kwenye semina ukiwa na mkakati wa kufanyia kazi.
Tano; siku hiyo ya semina, usitumie kabisa mtandao wowote wa kijamii, na nakuhakikishia hakuna utakachopoteza zaidi ya kupata muda, utulivu na umakini zaidi.
Karibu sana tarehe 03/11/2018 tufanye zoezi hili kwa pamoja, zoezi ambalo litakusaidia sana kwenye maisha yako.
Kama bado hujapata nafasi yako ya kushiriki semina ya KISIMA CHA MAARIFA 2018, imebaki siku moja tu ya kupata nafasi hii.
KARIBU KWENYE SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018.
Rafiki, tarehe 03/11/2018 ndiyo siku ya SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, semina hii itafanyika kwenye moja ya hoteli zilizopo jijini dar es salaam.
Itakuwa ni semina ya siku nzima, kuanzia saa moja asubuhi mpaka saa moja jioni. Yatakuwa ni masaa 12 ya kujifunza, kujuana na wengine, kuhamasika na kuweka mkakati wa kwenda kufanyia kazi kwa mwaka mzima.
Ada ya kushiriki semina hii ni tshs 100,000/= (laki moja) ada ambayo itajumuisha huduma zote za siku ya semina, kuanzia chai, chakula cha mchana, vitafunwa vya jioni, vijitabu vya kuandikia na kalamu.
Ili kupata nafasi ya kushiriki semina hii, unapaswa kulipa ada yako kabla ya tarehe 31/10/2018, ambayo ndiyo tarehe ya mwisho ya kulipia ada.
Pia nafasi za kushiriki semina hii ni 100 pekee, na zilizobaki ni chache sana. hivyo kama hutaki kukosa nafasi hii, lipa ada yako mapema ili tuweze kuwa pamoja kwenye semina hii.
Nakusubiri kwa hamu sana rafiki yangu kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, kwa sababu yapo mengi mazuri nimekuandalia kwa mafanikio yako kwa mwaka 2018/2019.
Namba za kufanya malipo ili kushiriki semina hii ni MPESA- 0755 953 887 au TIGO PESA/AIRTEL MONEY – 0717 396 253. Majina ya namba hizo ni AMANI MAKIRITA. Ukituma fedha tuma na ujumbe wa kueleza umefanya malipo ya semina, ukiambatana na jina lako na namba yako ya simu kwa ajili ya kupewa taarifa zaidi za semina.
Karibu sana siku ya tarehe 03, ili tuweze kufanya majaribio haya matano kwa pamoja. Kamilisha malipo yako leo ili usikose nafasi hii bora sana ya kuyaboresha zaidi maisha yako.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL