Rafiki yangu mpendwa,

Kwa wastani, kila mmoja wetu anatumia zaidi ya theluthi mbili ya maisha yake akiwa macho, yaani anakuwa hajalala. Na zaidi ya theluthi moja ya maisha yetu tunaitumia kwenye kazi au biashara ambazo tunafanya. Hivyo kila tunachofanya kwenye maisha yetu, kina mchango mkubwa sana kwenye hali yetu ya furaha na ubora wa maisha pia.

Kuna watu ambao wapo kwenye kazi au biashara ambazo ni nzuri sana, ambazo ukiziangalia kwa nje wewe mwenyewe unatamani ungekuwa unafanya wanachofanya. Lakini watu hao wanakuwa hawana furaha kabisa na kile wanachofanya. Watu hawa mara zote wanakuwa na msongo wa mawazo na maisha yao hayawi bora, wanakosa furaha kwenye maisha yao.

Kwa upande wa pili, wapo watu ambao wanafanya kazi ambazo zinaonekana ni za hovyo na za kujirudia sana, kazi ambayo wengine wakiangalia kwa nje wanaidharau na kuona haina ufahari kufanya. Lakini unakuta watu hao wanafurahia sana kazi wanayoifanya, wanaifanya kwa ubora na maisha yao yanakuwa ya furaha na yanakuwa bora zaidi.

Wanasaikolojia wamekuwa wakijiuliza kwa muda mrefu ni nini kinachangia baadhi ya watu kupenda na kufurahia vitu ambavyo ni vya kawaida na wengine kudharau vitu ambavyo ni vizuri.

Mwanasaikolojia Mihaly Csikzentmihalyi alikuja na jibu la swali hili kwenye kitabu chake kinachoitwa Flow: The Psychology of Optimal Experience. Kitabu hiki  kimeeleza kwa kina kwa nini baadhi ya watu wanafurahia kile wanachofanya wakati wengine hawafurahii. Na pia kwa mtu binafsi, kwa nini kuna wakati unafurahia kufanya vitu fulani na vingine hufurahii kufanya.

workflow

Kwa mfano umewahi kuwa unafanya kitu na ukajikuta unafurahia sana kukifanya na hutaki kuacha kabisa kukifanya, unajikuta hufikirii kitu kingine na hata muda hujui unaishaje, yaani ni kama unajikuta siku imeisha na hujui imeishaje. Wakati kitu kingine hujisikii kabisa kukifanya, unaona kama muda hauendi na huwezi kuituliza akili yako hata kwa muda mfupi ili ufanye kitu hicho.

Kupitia kitabu cha Flow, mwandishi anatushirikisha njia ambayo tunaweza kuitumia na tukafurahia chochote ambacho tunakifanya na hata kuwa na maisha yenye furaha. Na mwandishi ameonesha kwa mifano jinsi ambavyo kila tunachofanya kwenye maisha yetu, hata kiwe cha kawaida kiasi gani, tunaweza kukifurahia sana na maisha yetu yakawa bora.

Hapa nakwenda kukushikisha hatua nane zitakazokuwezesha kufurahia chochote unachofanya na kuyawezesha maisha yako kuwa bora sana. Na ninaposema chochote, namaanisha chochote kweli, hata kama ni kuosha vyombo au kufagia uwanja, unaweza kufurahia chochote unachofanya na maisha yako yakawa bora sana.

Zifuatazo ni hatua nane za kufurahia chochote unachofanya na kuwa na maisha bora na yenye furaha.

Hatua ya kwanza; uwezekano wa kukamilisha unachofanya.

Hatua ya kwanza ya kufurahia chochote unachofanya ni kuwepo kwa uwezekano wa kukamilisha kile unachofanya. Pale unapofanya kitu ambacho unajua matokeo ya mwisho na unaweza kuyafikia, unakuwa na furaha sana pale unapokikamilisha. Lakini kama utafanya kitu ambacho huwezi kukikamilisha, ni rahisi kuona kama siyo kitu kikubwa. Na kama unachofanya hakimaliziki, basi unaweza kukigawa kwa hatua ndogo ndogo ambazo unaweza kuzikamilisha kwa wakati.

Hatua ya pili; uwezo wa kuweka umakini wako wote kwenye kile unachofanya.

Umakini wako wote unapaswa kuwa kwenye kile ambacho unakifanya. Usiruhusu mawazo yako kwenda kwenye kitu kingine tofauti na kile unachofanya. Watu wengi hawafurahii kile wanachofanya, kwa sababu wanapokuwa wanafanya, mawazo yao yanakuwa kwenye vitu vingine tofauti na kile wanachofanya. Lazimisha mawazo yako yote yawe kwenye kile unachofanya na utaweza kukifurahia sana.

SOMA; Fanya Majaribio Haya Matano (05) Ndani Ya Siku Moja Na Maisha Yako Yatakuwa Bora Sana.

Hatua ya tatu; malengo ambayo yako wazi na yanaeleweka.

Kile unachofanya, lazima kuwe na malengo ambayo yako wazi na yanaeleweka. Lazima ujue wapi unapoanzia na wapi unapoishia. Bila ya kuwa na malengo ya wazi itakuwa vigumu kujua kipi muhimu zaidi kufanya na hata unapokamilisha, hutajua kama umekamilisha. Malengo kwenye kile unachofanya ni muhimu, ndiyo yatakayokuongoza na kukusukuma kufanya zaidi.

Hatua ya nne; uwepo wa mrejesho wa haraka.

Unapokuwa na mrejesho wa haraka kwenye kile unachofanya, ni rahisi kuona kama uko kwenye njia sahihi au umeshaondoka kwenye njia sahihi. Kila unachofanya unapaswa kuwa na njia ya kujipima mwenendo wako na pale mwenendo unapokuwa mzuri unapata furaha. Hata kama mwenendo siyo mzuri, utapata nafasi ya kujirekebisha.

Hatua ya tano; uwepo wa ugumu unaokutaka ujitume zaidi.

Kile unachofanya, kikiwa rahisi na chepesi sana kufanya, huwa hatupati raha ya kukifanya. Lakini kunapokuwa na ugumu ambao unatufanya tujitume zaidi, tunafurahia kitu hicho. Kadiri kitu kinavyokuwa kigumu, lakini ndani ya uwezo wetu wa kukifanya, ndivyo tunavyojisukuma kukifanya zaidi. Na katika kujisukuma huko unasahau hofu mbalimbali ambazo zinawasumbua wale ambao hawana ugumu kwenye yale wanayofanya.

Hatua ya sita; kuwa na udhibiti kwenye hatua unazochukua.

Kitu kingine kinacholeta furaha kwenye kile unachofanya ni kuwa na udhibiti wa hatua unazochukua. Pale ambapo unafanya kitu kwa sababu umechagua kufanya na unajua ni muhimu sana kwako kufanya unakifanya kwa kujituma na unafurahia unachofanya. Lakini pale unapokosa udhibiti, pale unapofanya kitu kwa sababu umelazimishwa kufanya, hufurahii kile unachofanya.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kusoma Vitabu Zaidi Ya 50 Kwa Mwaka Hata Kama Huna Muda Au Fedha Za Kununua Vitabu Vingi.

Hatua ya saba; unaacha kujifikiria wewe mwenyewe.

Katika kufanya kile ambacho umechagua kufanya, umakini wako wote unakuwa kwenye kile unachofanya kiasi kwamba unaacha kujifikiria wewe mwenyewe. Ni kama unajisahau kabisa wewe mwenyewe na kufikiria kile ambacho unakifanya tu. Hali hii inakufanya uwe na umoja na kile unachofanya na ufurahie sana. Na unapomaliza kufanya, unakuwa bora sana wewe binafsi kuliko ulivyokuwa kabla hujaanza kufanya.

Hatua ya nane; dhana ya muda inapotea.

Unapokuwa unafanya kitu ambacho umakini na mawazo yako yote umeyaweka pale, dhana ya muda kwako inapotea kabisa. Hujiulizi ni muda gani umepita na unaona kama muda unaruka, kwa sababu unaona kama umefanya kwa muda mfupi lakini unakuta muda umeenda sana. Unaweza usikumbuke kama umekula au la, kwa sababu kazi inakuwa imekumeza kabisa.

Rafiki, hatua hizi nane kwa pamoja zinaleta furaha kubwa kwa mtu kupitia kile ambacho anafanya. Kwenye kila unachofanya kwenye maisha yako kuanzia sasa, weka hatua hizi nane na utaona jini ambavyo maisha yako yatakuwa bora sana. Na hatua muhimu sana unazopaswa kuweka kwenye chochote unachofanya ni kuwa na lengo ambalo linakusukuma zaidi, kuwa na mrejesho kwenye kila hatua unayopiga, kuwa na udhibiti wa hatua unazochukua, weka umakini wako wote kwenye kile unachofanya na jisahau kabisa katika kufanya kile ulichochagua kufanya, hicho pekee ndiyo kichukue muda na umakini wako.

Kwa kufuata hatua hizi, kila unachofanya, kuanzia kazi, biashara, kula, kupumzika, kufanya mapenzi na hata kusoma kutakuwa kwa furaha kubwa sana kwako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge