Zipo aina kuu mbili za thamani unazopaswa kuzijua na kuzifanyia kazi kila siku kwa ajili ya mafanikio yako.
Aina ya kwanza ni thamani ya fedha, hii ni thamani ambayo watu wanalipa kwa fedha. Kama unalipa elfu kumi, thamani ya fedha hiyo ni elfu kumi.
Aina ya pili ni thamani ya matumizi, hii ni thamani ambayo mtu anaipata kwa kutumia kitu fulani. Kama mtu amenunua kitu ambacho kinayafanya maisha yake kuwa bora sana, basi kitu hicho kina thamani kubwa ya matumizi kwake.
Je unatumiaje thamani hizi mbili kwa mafanikio yako?
Tumia kanuni hii kila siku; toa thamani kubwa ya matumizi kuliko thamani ya fedha unayochukua.
Yaani kwenye chochote unachofanya, wape watu thamani kubwa ya matumizi, kuliko thamani ya fedha wanayokupa. Kwa maneno mengine unapaswa kutoa zaidi ya unavyolipwa. Wafanye watu waone wamenufaika zaidi ya walivyolipia.
Kwa kufanya hivi watu watakutegemea na watakuamini sana na hutakosa watu wa kukulipa kwa kile unachofanya.
Kabla hujaangalia unalipwa nini, angalia kwanza unatoa nini. Angalia kama kile unachofanya kinaongeza thamani kwenye maisha ya wengine, angalia kama kinayafanya maisha yao kuwa bora zaidi.
Mara zote kazana kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi kuliko yalivyokuwa. Mfanye kila anayekutana na wewe au kazi zako aondoke wakiwa bora zaidi ya alivyokuwa awali. Kwa njia hii hutakuwa na shaka juu ya kiasi unacholipwa, kwa sababu kitakuwa kingi sana.
Hakuna mtu anayetoa thamani kubwa na akawa na tatizo la kipato, kipato chako ni matokeo ya thamani unayotoa kwa wengine.
Kazana kutoa thamani kubwa ya matumizi kuliko unayochukua kwenye fedha na hilo litakufanya uweze kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,